Mvutano waibuka baraza la wawakilishi Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:11 PM Jun 18 2026
news
Picha Rahma Suleiman
Mvutano waibuka baraza la wawakilishi Zanzibar

Mvutano wa kisiasa umeibuka katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar baada ya wajumbe wa ACT Wazalendo kutokuwepo ukumbini wakati wa hatua za mwisho za kupitishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027.

Akizungumza na Nipashe Didigital, Mnadhimu wa Wajumbe wa ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakihi, amesema wajumbe wa chama hicho waliondoka baada ya kuona mjadala wa bajeti haukuwa wa haki na haukutoa nafasi ya kutosha kwa mawazo ya upinzani kusikika.

“Tulikuwa na hoja nyingi muhimu za kuwasilisha lakini baadhi ya wajumbe tuliowapendekeza hawakupewa nafasi ya kuchangia. Tuliona uwepo wetu usingebadilisha chochote kwa sababu mjadala ulikuwa ukidhibitiwa na upande mmoja,” amesema Prof. Fakihi.

Ameongeza kuwa ACT ilitaka kutumia mjadala huo kueleza wananchi kuhusu baadhi ya mapungufu wanayoyaona katika bajeti hiyo, lakini haikupata fursa ya kufanya hivyo kikamilifu.

Hata hivyo, Mnadhimu wa Wajumbe wa CCM, Machano Othman Said, amepinga madai hayo akisema ACT haina sababu za msingi za kulalamika kwani ilipewa nafasi ya kushiriki mjadala huo.

“CCM ina wajumbe 66 kati ya 80 wa Baraza, wakati ACT ina wajumbe 14. Kwa uwiano huo haiwezekani idadi ya wachangiaji ikawa sawa. ACT walipata nafasi ya kuchangia kupitia wajumbe kadhaa, hivyo madai yao hayana msingi,” amesema Machano.

Amesema ACT haikuwasilisha majina ya wachangiaji siku ya kwanza ya mjadala na kwamba hata hivyo waliruhusiwa kushiriki kutokana na kuzingatia mfumo wa vyama vingi.

Wakati ACT ikidai haki ya kutoa maoni haikuzingatiwa ipasavyo, CCM inasisitiza kuwa taratibu za Baraza zilifuatwa. Mvutano huo unaendelea kuibua mjadala kuhusu ushiriki wa upinzani katika mijadala muhimu ya kisera na bajeti Zanzibar.