Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewata wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule zinazotoa elimu ya amali na mafunzo ya ufundi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Mwajuma Lingwanda, wakati akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba.
Kwa mujibu wa Mwajuma, mafunzo ya ufundi ndiyo njia ya kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi yatakayochochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
Amesema NACTVET imetumia maonesho hayo kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa ushauri kuhusu uanzishaji wa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na huduma nyingine zinazopatikana katika ofisi za baraza hilo.
"Tumeridhishwa na mwitikio wa wananchi wanaotembelea banda letu. Wengi wamepata taarifa na huduma walizokuwa wanazihitaji, na tunaamini wataendelea kuwafikishia wengine ujumbe kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya elimu ya ufundi," alisema.
Amesema moja ya vivutio vikubwa katika banda la NACTVET mwaka huu ni ushiriki wa wanafunzi wa shule za amali wanaoonesha kwa vitendo ujuzi walioupata darasani kupitia kazi mbalimbali wanazozifanya.
"Hawa vijana wanaonesha uwezo wao kutokana na mafunzo waliyopata. Hii ni ishara kuwa elimu ya amali inawajengea uwezo wa kufanya kazi na kuzalisha mara tu wanapomaliza masomo," amesema.
Mwajuma amesema mafunzo ya ufundi na elimu ya amali yana mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kujiajiri, kuajiriwa, kubuni teknolojia na kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini.
Amewahimiza wawekezaji na wadau wa elimu kutumia fursa zilizopo kuanzisha shule na taasisi zinazotoa mafunzo ya amali na ufundi stadi, akisema NACTVET ipo tayari kutoa ushauri na kuelekeza taratibu zote zinazohitajika.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED