Rais Tshisekedi kufanya ziara ya kikazi Z'bar

By Gwamaka Mwaipungu , Nipashe
Published at 10:35 AM Aug 18 2026
Rais Tshisekedi kufanya ziara ya kikazi Z'bar
Mtandao
Rais Tshisekedi kufanya ziara ya kikazi Z'bar

RAIS wa Jamhuri ya Congo, Felix Tshisekedi anatarajiwa kuwasili Zanzibar leo, Jumatatu Agosti 17, 2026, majira ya saa moja usiku kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, katika ziara inayotarajiwa kuongeza nguvu katika uhusiano wa Tanzania na Jamhuri ya Congo.

Ziara hiyo inakuja wakati Zanzibar ikiendelea kuwa mwenyeji wa shughuli mbalimbali zinazohusisha viongozi na wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku eneo la Kizimkazi likiwa kitovu cha shughuli za kitaifa na kimataifa katika kipindi hiki.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, kesho Jumanne Agosti 18, 2026, Rais huyo wa Congo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, huko Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kujikita katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Congo, pamoja na masuala ya maendeleo, biashara, uwekezaji na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja.

Ujio wa Rais huyo Zanzibar pia unaipa Kizimkazi nafasi nyingine muhimu katika diplomasia ya Tanzania, baada ya eneo hilo kutumika katika shughuli mbalimbali za kitaifa zinazohusisha Rais Samia.

Kizimkazi inayopatikana Mkoa wa Kusini Unguja, imeendelea kujijenga kama eneo lenye umuhimu katika sekta za utalii, uchumi wa buluu, uwekezaji na shughuli za kitaifa, hivyo mazungumzo ya viongozi hao yanatarajiwa kuongeza uzito wa kimkakati katika matumizi ya fursa hizo.

Ziara hiyo pia inatazamwa kama fursa ya kuendeleza diplomasia ya Tanzania barani Afrika, hususan katika kujenga mahusiano yanayoweza kufungua milango ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya mataifa hayo mawili.

Rais Dk Samia amekuwa akisisitiza umuhimu wa diplomasia ya kiuchumi katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo, huku Tanzania ikiendelea kushirikiana na nchi mbalimbali za Afrika katika masuala ya maendeleo.

Kuwasili kwa Rais wa Congo Zanzibar na mazungumzo yake na Rais Samia huko Kizimkazi kunatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio muhimu ya kidiplomasia yanayofanyika Tanzania katika kipindi hiki.