Zanzibar inatarajiwa kuandika ukurasa mpya katika historia ya siasa zake baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutarajiwa kushuhudia hafla ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.
Hafla hiyo ya kihistoria inatarajiwa kufanyika Julai 9, 2026, saa 4:00 asubuhi katika viwanja vya Ikulu, Zanzibar, ikiwa na lengo la kuimarisha maridhiano, mshikamano wa kitaifa, utulivu wa kisiasa na amani endelevu visiwani humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu, tamko hilo linatokana na maafikiano yaliyofikiwa na vyama hivyo viwili vikuu vya siasa, yakilenga kujenga msingi imara wa ushirikiano katika masuala ya kitaifa na maendeleo ya wananchi.
Katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi atakuwa pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambapo watashuhudia uwasilishaji wa tamko hilo pamoja na utiaji saini wa ajenda mbalimbali zilizokubaliwa kwa ajili ya utekelezaji wake.
Hafla hiyo inatarajiwa kukutanisha viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wawakilishi wa taasisi mbalimbali pamoja na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hafla hiyo pia itarushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ili kuwapa wananchi nafasi ya kushuhudia tukio hilo muhimu.
Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa linatarajiwa kuwa alama ya mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano kati ya wadau wa kisiasa, huku likiweka mbele maslahi ya taifa, umoja wa wananchi na ustawi wa Zanzibar.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED