Wizara ya Katiba na Sheria imewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda la wizara hiyo ili kupata huduma ya msaada wa kisheria bila malipo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba, alipotembelea banda la wizara hiyo katika maonesho yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katimba amesema katika kipindi chote cha maonesho hayo, jopo la wataalamu wa sheria litakuwa likitoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kwa kusikiliza migogoro yao na kuwapa ushauri pamoja na mwongozo wa namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote wenye changamoto za kisheria kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili wapatiwe huduma za msaada wa kisheria bila malipo,” amesema Katimba.
Aidha, amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro, akieleza kuwa pamoja na mahakama kuwa na mamlaka ya kikatiba ya kusimamia upatikanaji wa haki, Serikali inaamini njia hizo zina mchango mkubwa katika kujenga maridhiano na kuimarisha mahusiano miongoni mwa wananchi.
“Tunaamini kuwa usuluhishi ni njia inayowafanya wenye migogoro waridhiane na kutoka wote wakiwa washindi, tofauti na mfumo wa mashauri mahakamani ambapo mara nyingi hupatikana mshindi mmoja na mwingine kushindwa,” amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED