Kocha wa Misri alalamika ‘tumeibiwa’ robo fainali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:02 PM Jul 08 2026
news
Picha Mtandao
Kocha wa Misri alalamika ‘tumeibiwa’ robo fainali

Kocha wa Misri, Hossam Hassan, amesema timu yake ‘imeibiwa’ nafasi ya kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kufungwa mabao 3-2 na Argentina katika mchezo uliogubikwa na utata wa uamuzi wa waamuzi wa VAR.

Misri ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 kabla ya Argentina kutoka nyuma na kupata ushindi uliwawezesha kutinga robo fainali, lakini Hassan anaamini matokeo hayo yaliathiriwa na uamuzi usio na haki.

"Sihitaji kuzungumza kuhusu bahati mbaya. Leo (jana) tumeibiwa waziwazi na tumetendewa dhuluma," alisema Hassan baada ya mchezo.

Utata ulianza kipindi cha kwanza baada ya bao la Mostafa Zico kufutwa kufuatia VAR kubaini kuwa kulikuwa na faulo dhidi ya Lisandro Martínez mwanzoni mwa shambulizi hilo.

Hata hivyo, Zico baadaye alifunga tena na kuipa Misri bao la pili, jambo lililoifanya timu hiyo kuwa karibu sana kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yake kwenda robo fainali ya Kombe la Dunia.

Kocha wa Misri, Hossam Hassan
Mjadala mkubwa zaidi ulitokea katika dakika za mwisho kabla ya bao la ushindi lililofungwa na Enzo Fernández. Wamisri wanaamini walipaswa kupewa penalti baada ya Alexis Mac Allister kudaiwa kumvuta jezi Hamdy Fathy ndani ya eneo la hatari.

"Hatujaoneshwa heshima wala haki. Penalti yetu haikutolewa na hata VAR haikuangalia tukio hilo. Pia tuliona bao letu likifutwa kwa namna ya kushangaza," alisema kocha huyo.

Hassan aliongeza kuwa amepoteza imani na mwenendo wa mashindano hayo kiasi  hataendelea kuyafuatilia.

ESPN