SEKTA binafsi nchini, inatarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Hayo yamesemwa juzi jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Green Climate Fund (GCF) ulioongozwa na Ofisa Mwandamizi eneo la Uwekezaji katika eneo la mabadiliko ya tabianchi, Mihir Sorti.
Ujumbe wa GCF ulifanya ziara yake nchini Tanzania kuanzia Agosti 11 hadi 14, 2026 na kukutana na wadau mbalimbali nchini wanaohusika katika eneo la fedha za mabadiliko ya tabianchi mkoani Simiyu na jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dk. Muyungi alisema kuna umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imebeba nguzo tatu muhimu.
“Pamoja na hayo, ushirikiano kati ya Serikali, GCF na sekta binafsi ni muhimu katika kuongeza uwekezaji wa miradi ya kijani, kuchochea ubunifu na matumizi ya teknolojia.
“Ushirikiano wa Serikali na GCF utaongeza upatikanaji wa fedha za tabianchi, hatua zitakazowezesha Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wenye pato la taifa linalofikia Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050,” alisema Dk. Muyungi.
Miongoni mwa nguzo tatu zinazounda Dira 2025 alizitaja kuwa ni pamoja na uchumi imara, jumuishi na shindani ambazo zinafungua fursa za kiuchumi na hivyo kuweka mazingira ya kupunguza umaskini na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote.
Nguzo ya pili ni uwezo wa watu na maendeleo ya jamii ambayo inalenga kuimarisha uwezo wa watu na ustawi wa jamii, ikiwa na dhamira katika kuleta usawa wa kijinsia kwa wote na kuwa na jamii jumuishi ili kutumia mbinu thabiti zinazoambatana na kudumisha maadili mema, kujenga hulka ya kujiamini na kujifunza bila ukomo.
“Uchumi imara utahakikisha kwamba, maendeleo ya kiuchumi yanawanufaisha wananchi wote na hivyo katika muktadha huu, Tanzania imeendelea kupiga hatua za kiuchumi na kukua kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa mwaka katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
“Yote hayo yanawezakana kupitia usimamizi endelevu wa mazingira ambao umetajwa pia kama nguzo ya tatu ambayo ni uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Muyungi, nguzo hiyo inazingatia umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali na usimamizi madhubuti ambao ni muhimu katika uhifadhi wa mazingira unaohusisha ulinzi wa bioanuai, usimamizi endelevu wa rasilimali maji na ardhioevu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED