Utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji katika Kata ya Mawenzi, Manispaa ya Moshi, unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji na kunufaisha wakazi zaidi ya 42,000 wa kata za Kaloleni, Njoro na Miembe, huku viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 wakisisitiza kukamilishwa kwa haraka ili kupunguza upotevu wa maji na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amesema chanzo hicho ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.
Amesema Serikali imewekeza fedha kuhakikisha chanzo hicho kinaboreshwa ili wananchi wengi zaidi waweze kupata huduma ya maji.
Hata hivyo, amesisitiza haja ya kukamilisha maeneo yenye upotevu wa maji ili kuongeza ufanisi wa mradi huo, akibainisha kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWASA) imeahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo ujenzi wa bomba na uzio ndani ya muda mfupi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MUWASA, Mhandisi Kija Limbe, amesema mamlaka hiyo kwa sasa huzalisha wastani wa mita za ujazo 43,322 za maji kwa siku, sawa na asilimia 60 ya mahitaji ya maji katika Manispaa ya Moshi.
Amesema kupitia mradi wa upanuzi wa chanzo hicho, uzalishaji utaongezeka kutoka mita za ujazo 750 hadi 3,840 kwa siku mara baada ya kukamilika, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya takribani shilingi milioni 600 na unalenga kunufaisha zaidi ya wakazi 42,000 wa kata za Kaloleni, Njoro na Miembe.
Mkazi wa Kata ya Njoro, Claudia Ruben, amepongeza mradi huo lakini akaomba serikali kuangalia upya gharama za bili za maji ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu huduma hiyo.
Mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030, inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED