Marekebisho sheria za kodi kusaidia utekelezaji Bima ya Afya kwa Wote

Nipashe
Published at 11:27 AM Aug 20 2026
Afisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Yusta Kaunda.
Frank Monyo
Afisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Yusta Kaunda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema marekebisho ya sheria za kodi yaliyoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27 yanalenga kuongeza mapato ya Serikali, yatasaidia kugharamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote nchini.

Ofisa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Yusta Kaunda alieleza hayo wakati wa semina kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

Alisema miongoni mwa mabadiliko hayo ni ongezeko la ushuru wa bidhaa wa Shilingi 20 kwa kila sigara 1,000.

Yusta alisema ongezeko hilo ni sehemu ya marekebisho yaliyofanywa kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2026, ambayo pia imehusisha marekebisho yanayohusiana na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura ya 161.

Alisema mapato yatakayokusanywa kutokana na ongezeko hilo la ushuru yameelekezwa kuwa chanzo maalum cha fedha kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.

Kwa mujibu wa Yusta, hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa serikali kugharamia huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa ufanisi zaidi.

Aidha, alisema marekebisho hayo yameunganisha utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na sheria zinazosimamia ushuru wa bidhaa, ikiwemo Sheria ya Ushuru, Sura ya 147, ili kuweka mfumo wa kisheria wa ukusanyaji na uelekezaji wa mapato hayo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wafanyabiashara Wilaya ya Nkasi, Willington Kiziba, aliishukuru TRA na Serikali kwa ujumla kwa maboresho hayo ya sheria, akisema yana umuhimu katika kuongeza mapato na kuchangia huduma zinazogusa maisha ya wananchi.