TARURA yatenga Mil 730/- kuboresha miundombinu Ifakara

By Christina Haule , Nipashe
Published at 11:15 AM Jul 08 2026
news
Picha Christina Haule
TARURA yatenga Mil 730/- kuboresha miundombinu Ifakara

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro imetenga kiasi cha Sh. milioni 730 ili kuboresha miundombinu mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara uliopo wilayani Kilombero.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Ndyamukama amesema kati ya fedha hizo Sh. milioni 400 zitatumika kukarabati barabara za mitaa katika mji wa Ifakara.

Amebainisha hayo jana katika mkutano wa hadhara mbele ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe.

“Sh. milioni 330 zitatumika kujenga Daraja la Mkasu lililopo Kiberege mradi ambao unatarajiwa kurahisisha mawasiliano na usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo,” amesema.

Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo na kufanya uwekezaji utakaochochea maisha ya wananchi wilayani humo.

Naye, Waziri Prof. Shemdoe amepongeza juhudi zinazofanywa na Rais Samia katika kuboresha kwa kasi shughuli za maendeleo nchini ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mkasu.