KIUNGO mshambuliaji Feisal Salum, leo anatarajia kukiongoza kikosi cha Azam FC kitakachocheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania.
Fei Toto Arusha leo kuipigania Azam
Na Mwandishi Wetu
KIUNGO mshambuliaji Feisal Salum, leo anatarajia kukiongoza kikosi cha Azam FC kitakachocheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania.
Feisal, maarufu kama Fei Toto amekuwa akihusishwa kuondoka kwenye kikosi hicho akitakiwa na klabu za Simba na Yanga, lakini habari za ndani kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema ataendelea kuwepo kwenye viunga vya Chamazi hadi mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapomalizika.
Azam itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kucheza dhidi ya Polisi Tanzania ambayo imerejea Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu iliposhuka msimu wa 2022/23.
Mchezo huo utapigwa saa 10:00 jioni, ambapo Azam itataka kuendeleza rekodi ya kushinda mchezo wa kwanza kama ilivyofanya msimu uliopita ilipoifunga Mbeya City mabao 2-0, Septemba 24 mwaka jana.
Wakati wenyeji watakuwa chini ya kocha Mbwana Makata, aliyeipandisha timu hiyo kwa njia ya 'play off' dhidi ya Prisons kwa kuichapa mabao 4-1, Azam itaongozwa na Mkongomani Florent Ibenge.
Kocha Ibenge amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na anauchukulia kwa umuhimu wa pekee mchezo huo kwani kushinda mechi ya kwanza kutatengeneza kujiamini kwa wachezaji wake.
Kocha Makata amekiri mchezo utakuwa mgumu kutokana na aina ya mpinzani anayekutana naye, lakini kwa sababu wanacheza nyumbani wanaamini wataibuka na ushindi licha ya kwamba bado ni wageni kwenye ligi.
Leo hii saa 12:30 kutakuwa na mchezo mwingine kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, wenyeji Coastal Union watakapoikaribisha Mashujaa FC kutoka mkoani Kigoma.
Coastal Union inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu iliyopita bao 1-0 kwenye uwanja huo huo, Septemba 17 mwaka jana dhidi ya Prisons ambayo imeshuka daraja.
Kwa upande wa Mashujaa yenyewe msimu uliopita ilianza kwa sare ya bao 1-1 nyumbani, Lake Tanganyika dhidi ya JKT Tanzania, Septemba 18 mwaka jana, leo hii inaanzia ugenini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED