Hadhari yatolewa El-Nino ikitarajiwa mwezi ujao

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:10 AM Aug 19 2026
Dkt. Ladislaus Chang’a akizingumza na waandishi wa habari hivi karibuni.
TMA
Dkt. Ladislaus Chang’a akizingumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha matarajio ya mvua kubwa itakayosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo nchini.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa uwezekano wa kutokea mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza kunyesha wiki ya nne ya mwezi Septemba katika mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka.

Akizungumza jana wakati wa kutoa utabiri wa mvua za vuli, Mkurugenzi wa TMA, Dk. Ladislaus Chang'a, alisema hali hiyo inaweza kusababisha madhara kwa binadamu, wanyama na mazingira, uharibifu wa miundombinu.

Alisema pia inaweza kuathiri utoaji wa huduma za kijamii, athari za kiuchumi na upotevu wa mali na kushauri Idara ya Menejimenti ya Maafa nchini kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Katika utabiri huo uliotolewa jana jijini Dar es Salaam, Dk. Chang'a. alisema kutokana na uwepo wa El-Niño, vipindi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2026 katika baadhi ya maeneo nchini.

Hata hivyo, alisema mvua za vuli, 2026 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2026 katika maeneo mengi na kutoa angalizo kutokana na uwepo wa El Niño kuelekea mwishoni mwa mwaka kunaweza kusababisha kuanza mapema kwa mvua za Novemba 2026 – Aprili 2027 (Msimu) katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, ambako kwa kawaida msimu wa mvua huanza mwezi Novemba.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara) pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo) ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani (mvua nyingi) katika maeneo mengi ya mikoa hiyo.

Maeneo mengine ni Ukanda wa Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani ikijumuisha Kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na Zanzibar ambapo mvua za juu ya wastani mpaka wastani zinatarajiwa wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2026 na kuisha mwezi Januari, 2027.

"Sekta, mamlaka husika, na kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji zinashauriwa kushirikiana na kuchukua hatua stahiki, ikiwa ni pamoja na kutoa tahadhari za mapema, kutoa elimu na miongozo itakayowezesha kuzuia au kupunguza madhara, kujiandaa, kukabiliana na maafa, na kurejesha hali endapo maafa yatatokea," alisema Dk. Chang'a.

Alisema athari nyingine zinazotarajiwa ni pamoja na ongezeko la kina cha maji katika mabwawa na mito hali ambayo inaweza kuathiri miundombinu ya rasilimali za maji na nishati.

"Lakini pia katika kipindi hiki, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji," alisema Dk. Chang'a.

SEKTA YA KILIMO

Alisema maeneo mingine yanatorajiwa kuathirika ni pamoja na kilimo na usalama wa chakula ambapo vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi kwenye udongo pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo.

Alisema magonjwa ya mazao yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi yanaweza kujitokeza. Magonjwa hayo yanaweza kuathiri ukuaji, ubora na mavuno ya mazao mbalimbali, hususani viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta pamoja na matunda na mbogamboga.

"Mvua za muda mrefu zinaweza kuathiri shughuli za uvunaji na kusababisha upotevu wa mazao baada kuvuna. Hata hivyo, shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama ilivyo kawaida katika baadhi ya maeneo katika msimu huu wa Vuli, 2026.

Alisema wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati," alisema Dk. Chang'a.

SEKTA YA UTALII

Mkurugenzi huyo alisema upatikanaji wa malisho na maji kwa wanyamapori katika mbuga na hifadhi za wanyamapori unatarajiwa kuwa mzuri.

Alisema hata hivyo, mvua nyingi zinazotarajiwa zinaweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko, ambayo yanaweza kusababisha wanyamapori kuhama.

Alisema hali hiyo inaweza kusababisha hatari ya magonjwa ya wanyamapori kusambaa kwa wanyama wanaofugwa, kutokana na wanyamapori kuingia katika maeneo ya jamii yanayozunguka mbuga na hifadhi, hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, na kusababisha hatari kwa binadamu na wanyama wanaofugwa.

SEKTA YA AFYA

Alisema magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji taka unaoweza kusababishwa na maji kutuama na kutiririka. Mamlaka zinazohusika na afya pamoja na jamii zinashauriwa kuchukua hatua stahiki za kiafya ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Alisema: "Hatua hizo ni pamoja na kutokomeza mazalia ya mbu, kuhakikisha upatikanaji wa akiba ya kutosha ya dawa na vifaa tiba, pamoja na kujiandaa kwa changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya usafiri, pia tunashauri vituo vya afya kuwa na mipango mbadala ya kuhakikisha mwendelezo wa huduma za afya"