Yanga yapigwa faini ya mlioni 100/- Hersi, Ntine kikaangoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:33 PM Jul 03 2026
Yanga.
Picha: Mtandao
Yanga.

Baada ya kurudia kosa, Yanga imetozwa faini ya Sh. milioni 100 kwa kosa la wachezaji na maofisa wake wa ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia nguo wakati wakicheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Pia Rais wa Yanga, Hersi Said na Ofisa Mtendaji Mkuu, Andre Ntine, wamepelekwa katika Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara walifanya kosa hilo siku ya mwisho wa kufunga pazia la ligi hiyo, mechi iliyomalizika wakiondoka na ushindi wa mabao 3-0.

Taarifa iliyotolewa leo na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi, imesema Yanga imepata adhabu hiyo kwa sababu ilitumia nyumba ya jirani kubadilishia nguo.

"Yanga imetozwa faini ya Sh.milioni 100 kwa kosa la wachezaji wake na maofisa wake wa ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaan, badala yake walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja, upande wa pili wa barabara kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:2 (2.5) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za michezo," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mara ya kwanza Yanga ilifanya kosa hilo  Mei 3, mwaka huu katika mechi ya dabi dhidi ya Simba iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.

Kamati hiyo ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu iliyokutaka jijini juzi pia imewatoza Mtibwa Sugar faini ya Sh. milioni tano kwa kosa la wachezaji wake na viongozi wa benchi la ufundi kutotumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo, katika mechi ya ugenini dhidi ya Namungo.