Yanga, Azam zatambiana kuelekea nusu fainali kesho

By Damian Masyenene , Nipashe
Published at 01:41 PM Jun 20 2026
news
Picha Damian Masyenene
Yanga, Azam zatambiana kuelekea nusu fainali kesho

Mabenchi ya ufundi ya klabu za Yanga na Azam FC yametambiana kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, utachezwa kesho katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza kuanzia saa 9:30 alasiri.

Wakizungumzia maandalizi ya vikosi vyao leo kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moalin amesema hawana hofu yoyote katika mchezo wa kesho kwakuwa anajivunia ubora wa nyota wake ambao tayari wameshacheza michezo mikubwa ya maamuzi na kubeba vikombe.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amekiri kuwa wapinzani wao, Yanga wamekamilika kila idara uwanjani kimbinu na kiufundi, lakini dhamira kuu ya kikosi chake ni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu.

‎Azam FC wataikabili Yanga kesho Jumapili kuanzia saa 9:30 alasiri, katika mchezo wa nusu fainali ya michuao hiyo, utakaochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

‎Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Moalin amesema maandalizi yao yanakwenda vizuri, na ni fahari kucheza nusu fainali, hivyo wachezaji wanatakiwa kufurahia mchezo huo bila presha yoyote kwakuwa wanahitaji kushinda na kwenda fainali.

‎"Wachezaji wetu wamekuwepo wamecheza michezo migumu na muhumu kama hii hapo kabla, wameshapata mafanikio makubwa, kitu cha kuwaambia ni kutuliza presha wacheze bila hofu wafurahie na wasichukulie poa mchezo huu, ili kile tulichokikusudia basi tukifanikishe," amesema Moalin.

Kadhalika, ‎Ibenge amesema wamejiandaa kwa namna ambayo wako tayari kucheza mchezo wa kesho, na lengo lao wanataka kwenda fainali.

‎"Yanga imekamilika, wako vizuri physical na technical, wanaweza kucheza kwa nguvu na kwa akili kwa sababu wana wachezaji wazuri, nasi tuna timu nzuri hivyo tunategemea mchezo bora zaidi wa nusu fainali," amesema Ibenge.

‎Amesema achezo huo utakuwa mgumu kwa sababu ni timu mbili zenye madaraja sawa, lakini wamefanya uchambuzia, kutazama video na kufanya kazi ya ziada kusahihisha makosa ya mechi zilizopita.

‎"Tunahitaji kufanya kazi ya ziada kuwa zaidi ya Yanga kiufundi, kimbinu, kisaikolojia na ndani ya uwanja. Kesho tunategemea matokeo mazuri," amesema Ibenge na kuongeza;

‎"Tuko vizuri mpaka sasa hatulalamiki, tuko mwisho wa msimu wachezaji wanakuwa wamechoka, tumebakiza michezo mitano lakini matarajio ni kufanya vizuri kila mchezo ulio mbele yetu."

‎Nahodha wa Azam FC, Himid Mao amesema ili kufanikisha dhamira yao ya kucheza fainali ya michuano hiyo ni lazima washinde mchezo huo.

1
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema limejipanga kuimarisha usalama kuelekea mchezo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema: “Tunatoa tahadhari kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kuingia au kusogea karibu na uwanja huo akiwa na silaha ya aina yoyote, ikiwemo silaha za moto, za jadi, au kifaa chochote chenye ncha kali kinachoweza kutumika kuumiza watu, isipokuwa kwa baadhi ya askari watakaokuwa na jukumu la kulinda usalama eneo hilo."