Imekuwa ni utamaduni wa kawaida kwa wadau mbalimbali wa michezo kupanga ratiba yake mapema ya wapi atakapokwenda kuangalia mechi hasa kipindi hiki cha mashindano makubwa ya Kombe la Dunia inayoanza leo.
Kuna ambao wanasema wanapenda kuangalizia nyumbani kwakuwa mechi nyingi zitaonyeshwa usiku, huku wengine wakisema wataangalizia kwenye vibanda umiza na wengine katika kumbi za starehe ambazo wenyewe wanachukulia kipindi hiki kama msimu wa mavuno.
Aidha, suala hilo limekuwa na mitazamo mseto kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo wengine wakisema hawawezi kuangalizia nyumbani kwasababu wanahitaji sehemu yenye shamra shamra (vibe) ili kupata burudani na ladha halisi ya michuano hiyo.
Hata hivyo, michuano hiyo mikubwa dunia, inaanza leo nchini Marekani, Mexico na Canada, huku sherehe za ufunguzi zikitarajiwa kufanyika kwa wakati mmoja katika maeneo tajwa.
Mechi ya kwanza, itakuwa kati ya Mexico na Afrika Kusini, kuanzia saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.
Timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni miongoni mwa mataifa 10 yanayowakilisha bara la Afrika katika mashindano hayo, huku Kocha wa DRC Sébastien Desabre, akisema vijana wa Leopard wamejiandaa vizuri.
"Tunaenda kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri katika michuano hii, wachezaji wametiwa moyo sana, wameahidi kupambana sana. Hatuna lingine, bali kufanya bidii. Tunalenga kufika katika hatua ya 32 bora." amesema kocha wa DRC.
Mbali na DRC mataifa mengine ya Afrika yanayoshiriki kwenye michuano hii ni pamoja na Morocco, Senegal, Algeria, Tunisia, Misri, Ivory Coast, Ghana, Cape Verde, na Afrika Kusini.
Kombe la dunia, linarejea tena nchini Marekani kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994, huku Mexico ikiwa mwenyeji baada ya kuandaa michuano hii mwaka 1970 na 1986, huku Canada ikianda michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Mechi 104 zitachezwa kwenye miji 16 katika nchi hizo tatu, huku mechi ya fainali ikitarajiwa kuchezwa Julai 19 jijini New York.
Kwa mara ya kwanza, timu zitakazoshiriki zimeongezeka kutoka 32 hadi 48.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED