Straika Singida aweka rekodi, wakaribia CAF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:58 PM Jun 18 2026
Winga wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe.
Picha: Mtandao
Winga wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe.

Winga wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe, amesema amefurahishwa kuwa mfungaji wa kwanza wa 'hat-trick' katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu na kuongeza itakuwa kumbukumbu kubwa kwenye maisha yake ya mpira wa miguu.

Nduwumwe alifunga mabao matatu (dakika ya 27, 35 na 84) katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa jana na kuifanya Singida Big Stars kuondoka na ushindi wa mabao 5-0.

Mshambuliaji huyo raia wa Burundi sasa amefikisha mabao 12, mawili nyuma ya kinara, Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye magoli 14 mpaka sasa.

"Nimefurahi sana, namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufunga 'hat-trick' katika mchezo huu, nawashukuru wachezaji wenzangu wote kwa kunifanya niweke rekodi hii.

Si rahisi kufanya hivi na mimi nimekuwa wa kwanza msimu huu, Ligi ya Tanzania ni ngumu na ya msimu huu ni ngumu zaidi kwa maana hiyo kazi kubwa imefanyika.

Nimepata pia tuzo hii ya uchezaji bora wa mechi, naipeleka kwa mashabiki wote wa Singida na viongozi wake," alisema nyota huyo.

Msimu uliopita jumla ya 'hat-trick' nne zifungwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Steven Mukwala na Jean Ahoua wote kutoka Simba, Stephane Aziz Ki na Prince Dube wa Yanga.

Nduwumwe alisajiliwa Singida Black Stars kipindi cha dirisha dogo akitokea Flambeau Du Centre FC ya Burundi na  amekuwa katika kiwango cha juu tangu atue nchini.

Ushindi huo umeifanya Singida Black Stars kujiimarisha katika nafasi ya nne ikifikisha pointi 47 ikifuatiwa na TRA United yenye pointi 41 na JKT Tanzania yenye pointi 38.

1