Simbu kujenga 'sports complex center ya riadha nchini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:21 PM Jun 11 2026
Bingwa wa dunia wa mbio za riadha za Tokyo, Japan mwaka 2025 aliyeshinda medali ya dhahabu. Felix Simbu, akizungumzia ndoto yake ya kujenga Athletics Sports Complex katika Mkoa wa Arusha.
Picha: Godfrey Mushi
Bingwa wa dunia wa mbio za riadha za Tokyo, Japan mwaka 2025 aliyeshinda medali ya dhahabu. Felix Simbu, akizungumzia ndoto yake ya kujenga Athletics Sports Complex katika Mkoa wa Arusha.

Bingwa wa dunia wa mbio za riadha, aliyeweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mbio ndefu za kilomita 42.195 mwaka 2025, Felix Simbu, ameanza rasmi kutimiza ndoto yake ya kujenga kituo maalum cha taifa kitakachoibua na kulea vipaji vya wanamchezo wa riadha.

Kupitia kampeni yake ya 'Kimbia na Simbu' kila hatua moja ya mguu wake itanunuliwa kwa Sh.1,000 ili kuinua vipaji vya wariadha wanaojifunza kwake kama role model (mfano wa kuigwa), huku sehemu ya fedha hizo zikitumika pia kujenga jengo la ghorofa tatu keneo la Ngateu, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.

Akizungumzia kampeni hiyo jijini Arusha, Simbu, amesema yeye pamoja na wenzake wanaokimbia na kuitangaza nchi nje ya mipaka yake, wanawaza ni kwa namna gani kizazi cha riadha cha Tanzania watachukua kwa mafanikio nafasi yao katika mchezo huo kitaifa na kimataifa.

"Mimi na wenzangu, Gabriel Geay yuko hapa ananisapoti mazoezini. Tunajaribu kuwaza, ni namna gani ambayo sisi tukifika mwisho wa kukimbia tutapata watu, wachezaji au wanariadha, ambao wataturithi na kuweza kuendelea kuipeperusha bendera yetu Watanzania vizuri.

...Wakati  tunaanza mbio, ilitokea gap (nafasi) hapa nchini hatukuwa na mwakilishi yeyote anayeliwakilisha nchi kimataifa. Ndio maana tumeanza. Naamini Watanzania wakitusapoti vizuri, tunaweza kufikia yale malengo na hatimaye kuzitimiza zile ndoto zetu."

Meneja wa Taasisi ya Simbu Foundation, Mosses Simon, amewaomba Watanzania kumuunga mkono Simbu katika kampeni hiyo ya hatua moja, Sh.1,000.
Kwa mujibu wa Mosses, maandalizi ya mashindano ya riadha yanahitaji rasilimali fedha na ushirikiano wa wadau mbalimbali, hivyo imeonekana ni vyema kuanzisha mfumo utakaowezesha wananchi wote kushiriki kwa kuchangia kulingana na uwezo wao.

“Tunataka kila Mtanzania akimbie pamoja na timu kuelekea ushindi. Sio lazima kukimbia barabarani, bali kushiriki kwa namna yoyote ile ya kuonyesha sapoti yake,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wakili John Manyama, amesema tayari shirikisho hilo limeanza kumuunga mkono Simbu, kwa kutuma wawakilishi wake kuangalia na kuchuja wanariadha chipukizi wenye vipaji katika mashindano ya michezo ya shule za msingi nchini (UMITASHUMTA) na mashindano ya michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA).

"Kama shirikisho, tumeanza kwa kuwatuma wawakilishi wetu waende katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA, ambavyo huko sasa unapata kujua kwamba kuna vipaji vya aina gani.Huko ndio unaweza kujua kwamba unahitaji rasilimali gani au rasilimali kwa kiwango gani  ili uweze ukaleta project mbalimbali katika medani ya riadha,"ameeleza Katibu huyo wa RT.