Samatta atangaza rasmi kustaafu kuichezea Stars

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:45 PM Jul 08 2026
news
Picha Mtandao
Samatta atangaza rasmi kustaafu kuichezea Stars

Wakati Tanzania inajiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani (AFCON 2027), kama mwenyeji wa mashindano hayo, nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu hiyo.

Samatta, straika wa Le Havre ya Ufaransa, amesema miaka 15 ambayo ameitumikia Taifa Stars na miaka 10 kama nahodha wa timu hiyo inatosha na sasa ni wakati wa kutoa nafasi kwa vipaji vipya.

Straika huyo wa zamani wa Simba, Samatta, alisema anawashukuru viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Serikali, familia yake, mashabiki pamoja na wadau wa soka nchini kwa kumuunga mkono wakati wote.

“Naamini huu ni wakati wa vipaji vipya kupewa nafasi ya kutufikisha kwenye hatua za juu zaidi,” Samatta aliyekuwa straika wa African Lyon ya Dar es Salaam na mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).

Licha ya kutangaza kuitumikia Stars, Samatta ameweka wazi ataendelea kutoa mchango kwa timu hiyo kupitia maeneo mengine ambayo yatakuwa ndani ya uwezo na uzoefu wake. 

“Ndugu Watanzania, asante sana kwa wakati wote tuliopambana pamoja katika wakati mzuri na ule uliotufunza, nimejivunia Utanzania wangu popote duniani nilipojaaliwa kufika, nimefurahia vipindi vyote nilipopata nafasi ya kuvaa jezi ya timu yangu ya taifa.

“Nimejaribu kadri niwezavyo kupambana kuwapa furaha. Kama inavyosemwa kila lililo na mwanzo halikosi mwisho, huu ndio mwisho wangu kama mchezaji kiwanjani, lakini sio mwisho wa mapenzi na sapoti yangu kwa Timu ya Taifa ya Tanzania.

“Tutakutana jukwaani kuwasapoti wanajeshi wetu. Asante Watanzania wenzangu,” alisema Samatta.