Perez aula tena Urais wa Madrid

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:23 PM Jun 08 2026
FLORENTINO Pérez.
Picha: Mtandao
FLORENTINO Pérez.

FLORENTINO Pérez ameshinda tena urais wa Real Madrid katika uchaguzi wa kwanza wenye upinzani wa kupiga kura tangu mwaka 2006.

Pérez alitangazwa mshindi hapo juzi katika hoteli karibu na Uwanja wa Bernabéu, huku mpinzani wake, Enrique Riquelme, akikubali kushindwa.

"Tumepata matokeo ya pili bora katika historia ya uchaguzi wa Real Madrid," alisema Pérez katika hotuba yake. 

"Ni matokeo ya ajabu... Leo (juzi), Real Madrid imeshinda. Tumeonesha mfano wa demokrasia kwa ulimwengu. Tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya Real Madrid ili kuendelea kushinda mataji... Nataka kumshukuru kila mtu aliyeshiriki. Kwa pamoja, tuna historia nyingi iliyobaki ya kutengeneza."

Katika uchaguzi huo, Pérez alipata kura 21,741 sawa na asilimia 65, huku Riquelme akipata kura 11,814 sawa na asilimia 35, tume ya uchaguzi ya klabu hiyo ilitangaza.

Pérez, mwenye umri wa miaka 79, amekuwa rais wa Real Madrid tangu mwaka 2009, na kabla ya hapo alikuwa kati ya mwaka 2000 na 2006.

Wakati wa Urais wake, Madrid imeshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara saba na idadi kama hiyo ya Ligi Kuu Hispania (LaLiga).

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kampeni ya wiki mbili iliyofuata uamuzi wa ghafla wa Pérez wa kuitisha mchakato huo, akitafuta uungwaji mkono kutoka kwa wanachama baada ya misimu miwili bila kombe kubwa.

Ulikuwa uchaguzi wa kwanza wenye ushindani ambao klabu hiyo ilikuwa imefanya katika kipindi cha miaka 20, huku Pérez akichaguliwa bila kupingwa mwaka 2009, 2013, 2017, 2021 na 2025.

Pérez tayari alikuwa ametangaza kurudi kwa José Mourinho kama kocha wa Madrid ikiwa atashinda uchaguzi wa Jumapili, pamoja na usajili wa Ibrahima Konaté na Denzel Dumfries, na ahadi ya kutoa zaidi ya euro milioni 150 kwa usajili wa mchezaji wa daraja la juu ‘Galáctico’ ambaye hakumtaja.