MAFUNZO ya waamuzi yaliyoratibiwa na Chama cha Soka Wilaya ya Nyang'hwale (NYADIFA) mkoani Geita, yamehitimishwa.
Yamewakutanisha washiriki 20 kutoka Wilaya za Chato, Bukombe, Geita na Nyang'hwale.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kuongeza idadi na ubora wa waamuzi nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa NYADIFA, Saimon Shija, amesema kuwa hatua hiyo inatekeleza dira ya maendeleo ya mpira wa miguu chini ya Rais wa TFF, Wallace Karia, kupitia mpango unaojulikana kama "Wallace Karia First Eleven."
Katibu wa Chama cha Waamuzi Mkoa wa Geita, Agustino Mapalala, amesema chama hicho kimejipanga kushirikiana na halmashauri mbalimbali kuhakikisha mafunzo kama hayo yanatolewa, ili kuongeza idadi ya waamuzi wenye sifa na kuimarisha kiwango cha uamuzi katika mashindano ya mpira wa miguu.
Christopher Chacha, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Grace Kingalame, amesema serikali inatambua nafasi muhimu ya waamuzi katika maendeleo ya mchezo wa soka, huku akiwataka washiriki kutumia maarifa waliyoyapata kusimamia sheria za mchezo kwa weledi, uadilifu na uzalendo.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya waamuzi wenye sifa na kuimarisha uwezo wao wa kutafsiri na kusimamia sheria za mchezo kwa weledi.
Hatua hiyo pia inaelezwa kuwa itachangia kuboresha uendeshaji wa mashindano ya soka katika ngazi za wilaya na mkoa, sambamba na kuibua fursa kwa waamuzi kufikia ngazi za juu zaidi za uamuzi nchini
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED