Hali mbaya ya hewa iliyoambatana na mvua kubwa ililazimisha mechi kati ya Ufaransa na Iraq iliyopigwa usiku wa kuamkia leo kusitishwa kwa muda wakati wa mapumziko kutokana na hofu ya kutokea kwa dhoruba na radi.
Licha ya yote hayo, mashabiki wa Iraq walionyesha matumaini wakiamini kuwa timu yao ingelifanya vizuri kama alivyoeleza Elie Jerjees.
"Unajua, watu wengi wanaidharau Iraq kwa sababu ni nchi ndogo, lakini tuko hapa kuishangaza dunia. Tayari tumefuzu kushiriki michuano hii na tulisubiri miaka 40 kurejea tena.
“Na tunaweza kupata matokeo mazuri zaidi. Tunaweza kufika raundi inayofuata. Tuna imani kubwa na timu hii. Tunafurahi sana kuwa hapa. Mvua haiwezi kutuzuia hata kidogo," amesema.
Katika mechi hiyo Ufaransa maarufu Les Bleues waliicharaza Iraq mabao 3-0 katika uwanja wa Philadelphia, ambako nyota wa Ufaransa Kylian Mbappé alifunga mabao mawili katika dakika ya 14 na 54 kabla ya Ousmane Dembele kupachika bao la tatu dakika ya 66.
Katika mechi nyingine ya usiku wa manane, Norway walichuana na Simba wa Teranga Senegal. Mchezaji Marcus Holmgren Pedersen wa Norway alipachika bao la kwanza katika dakika ya 43 kabla ya kwenda kwenye mapumziko.
Mechi hiyo ilimalizika kwa ushindi wa Norway kwa mabao 3-2 katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Katika mechi nyingine Argentina walipata ushindi wa mabao 2 - 0 dhidi ya Austria.
Mabao yote mawili yakifungwa na mchezaji nyota Lionnel Messi katika dakika ya 38 na 95 ambaye licha ya kushindwa penati ameweka rekodi ya kipekee ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika Kombe la Dunia baada ya kufunga bao lake la 18 kwenye michuano hiyo.
Mashabiki wa Austria hawakutarijia ushindi dhidi ya Argentina lakini wameonekana kuridhishwa na namna timu yao imeonyesha ujasiri uwanjani kwa kuepuka mvua ya mabao huku wakipambana kutafuta kusawazisha bila mafanikio.
Rais wa Austria Alexander van der Bellen, amesema kuwa ni fahari kwa timu hiyo kushiriki tena michuano hiyo.
"Hili ni jambo la kipekee. Kwa mara ya kwanza katika miaka 28, tumerudi kwenye Kombe la Dunia. Nitoe shukrani kwa timu nzima, lakini haswa kwa Ralf Rangnick, kocha ambaye aliweza kwa namna fulani kuyaratibu yote haya," amesema
Hata hivyo, ratiba ya mechi za leo ni kwamba Ureno ya Christiano Ronaldo watapambana na Uzbekistan huku England wakimenyana na Ghana.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED