Shabiki maarufu wa soka na mwanachama wa klabu ya Yanga kutoka Mkoa wa Geita, Hussein Makubi ameahidi kutoa zawadi ya Sh. 500,000 kwa kila goli litakalofungwa na timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, katika mchezo wa fainali ya AFCON U-17 dhidi ya Senegal utakaochezwa leo.
Mwanyanzala amesema hayo leo wakati akizungumza na Nipeshe Digital ambako amesema ahadi yake hiyo ni sehemu ya kuwapa motisha vijana hao ambao wameonyesha kiwango cha juu cha mchezo na kuiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano hayo.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, amesema lengo lake ni kuongeza morali kwa wachezaji kabla ya pambano hilo muhimu, huku akieleza kuwa ana imani kubwa na uwezo wa Serengeti Boys kufanya vizuri na kuandika historia mpya katika soka la vijana nchini.
“Niisisitize serikali kuendelea kulinda na kuendeleza vipaji vya vijana hao kwa kuweka mazingira bora yatakayowasaidia kukua kisoka na kufikia viwango vya kimataifa,” amesema.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Serengeti Boys yanapaswa kuwa chachu ya uwekezaji mkubwa zaidi katika maendeleo ya soka la vijana nchini Tanzania, ili kuibua kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kushindana katika ngazi za kimataifa.
Imeandikwa na Joel Maduka
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED