MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ameiahidi timu ya Dar City Basket kiasi cha Sh. milioni 50 endapo timu hiyo itafanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali katika mashindano yanayofanyika Kigali, Nchini Rwanda.
Akizungumza leo Mei 20, 2026 katika uwanja wa ndege wa Der es Salaam wakati wa kuiaga timu hiyo, Chalamila amesema mafanikio ya timu hiyo yatakuwa fahari kwa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
Pia amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuwafikisha vijana wenye vipaji vya mpira wa kikapu ofisini kwake ili kusaidia kukuza vipaji hivyo na kuwaunganisha na wachezaji wakubwa wa timu hiyo.
“Baada ya kurejea kutoka Rwanda, Rais wa timu hiyo Hashimu Thabit apange kikao na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadili uwezekano wa kujenga uwanja mkubwa na wa kisasa wa mpira wa kikapu,” amesema.
Aidha, Chalamila alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo, akisisitiza kuwa michezo ni afya lakini pia ni sehemu muhimu ya uchumi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED