AFCON, Tamasha kuchochea utalii Arusha

By Allan Isack , Nipashe
Published at 10:30 AM Jul 06 2026
"Tumeandaa tamasha hili kwa lengo la kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa sanaa na utamaduni, huku tukiwajengea vijana ujuzi na maarifa ya kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hizo," amesema Jama.
Picha: Allan Isack

Maandalizi ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yameanza kulichangamsha Jiji la Arusha, huku Tamasha la Kimataifa la Arusha Artisan Festival likitarajiwa kuongeza kasi ya utalii, ajira na biashara kupitia sekta ya sanaa na utamaduni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Jama, amesema tamasha hilo litafanyika Oktoba mwaka huu na linatarajiwa kuwavutia zaidi ya watalii 2,500 kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema tamasha hilo litakuwa la kwanza nchini kuunganisha sekta za utalii, sanaa na utamaduni kupitia maonesho ya wazi pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, hatua inayolenga kuitangaza Tanzania kimataifa na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa vijana.

"Tumeandaa tamasha hili kwa lengo la kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa sanaa na utamaduni, huku tukiwajengea vijana ujuzi na maarifa ya kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hizo," amesema Jama.

Ameongeza kuwa tamasha hilo litawakutanisha wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mitindo, wafinyanzi, wafumaji, wajasiriamali, wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari, taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau wa maendeleo.

Jama amesema tamasha hilo pia litaweka msingi wa kutambua na kuhesabu wasanii wa sanaa nchini, hatua itakayowezesha Serikali na wadau kupanga mikakati bora ya kuendeleza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Rukia Walele, amesema tamasha hilo linafungua ukurasa mpya wa kuitangaza sekta ya sanaa za ufundi, ambayo imeendelea kuchangia uchumi na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania.

Naye Mshauri wa Kiufundi wa Arusha Artisan Festival, Andrew Bumba, amesema tamasha hilo litakuwa kichocheo cha ajira kwa vijana kwa kuwaunganisha moja kwa moja na sekta ya utalii pamoja na masoko ya ndani na kimataifa.

Aidha, waandaaji wameeleza kuwa kuandaliwa kwa tamasha hilo sambamba na maandalizi ya AFCON kunatarajiwa kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Arusha na kuimarisha nafasi ya mkoa huo kama kitovu cha utalii katika Kanda ya Kaskazini.