MASHINDANO ya ya mwaka huu ya Imbeju Ndondo Cup 2026 yamepigwa tafu kubwa baada ya kupatikana mfadhili wa kuyafanikisha kufanyika mwaka huu.
Kiasi cha Shilingi Milioni 400 kimetangwa na Benki ya CRDB kupitia taasisi ya 'CRDB Bank Foundation' ili kuyafanikisha msimu huu ambapo fedha hizo zitatumika kuyaendesha pamoja na zawadi kwa washindi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, TullyEsther Mwambapa, alisema zaidi ya Sh milioni 100 kati ya fedha hizo zitatumika kama zawadi kwa mabingwa, washindi wa pili pamoja na tuzo mbalimbali kwa wachezaji na mashabiki.
Tully alisema msimu huu una fursa nyingi kwa wadau wote wanaoshiriki mashindano ya Imbeju Ndondo Cup.
Alieleza kuwa mabingwa wa mashindano hayo watajinyakulia Sh.30 milioni huku washindi wa pili wakiondoka na Sh. 20 milioni.
Kwa mujibu wa Tully, timu zitakazoshiriki pia zitakuwa zikipata zawadi za fedha katika kila hatua zitakayofanikiwa kufuzu, huku kiasi husika kikitarajiwa kutangazwa baadaye.
Aliongeza kuwa mchezaji bora wa mashindano (MVP) atazawadiwa Shilingi milioni mbili, huku mfungaji bora, beki bora na golikipa bora kila mmoja akipata Shilingi milioni moja.
Aidha, kutakuwa na zawadi ya Shilingi 100,000 kwa mchezaji bora wa mechi katika kila mchezo, pamoja na shabiki au kundi la mashabiki litakaloonyesha ushangiliaji bora zaidi.
“Fedha hizi zote zitawekwa kwenye Akaunti za Imbeju za washindi husika, jambo litakalowapa fursa zaidi za maendeleo na kuakisi kaulimbiu ya Imbeju Ndondo Cup 2026 ya ‘Jiongeze’,” alisema Tully.
Alibainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yameandaliwa kwa lengo la kutengeneza fursa kwa timu na wachezaji wa ngazi ya chini ili waanze safari ya kujikwamua kiuchumi kupitia vipaji vyao.
“ Tunathamini sana ubora. Ndiyo maana tumeweka mkazo katika kuwazawadia wote watakaoonyesha kiwango bora, iwe ndani ya uwanja au jukwaani, kwa kutambua mashabiki na vikundi vya ushangiliaji vinavyofanya vizuri zaidi,” alisema.
Tully aliongeza kuwa mbali na kufurahia soka, vijana watakaoshiriki watapatiwa mafunzo ya elimu ya fedha na kufunguliwa Akaunti za Imbeju zitakazowasaidia kusimamia mapato yatokanayo na vipaji vyao.
Pia watapatiwa mafunzo kuhusu uwekezaji, ujasiriamali, ubunifu na fursa mbalimbali zilizopo katika uchumi wa kisasa.
Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo, Yahaya Mohamed Mkazuzu, alisema mashindano hayo tayari yamewasaidia vijana wengi kufikia mafanikio kupitia mchezo wa soka.
Mkazuzu aliwataja baadhi ya wachezaji waliopata fursa ya kuchezea klabu kubwa baada ya kuonekana kupitia mashindano hayo ni pamoja na Idd Selemani Nado, Kelvin Sabato na Mashaka Pobga.
“Nawashukuru CRDB Foundation kupitia Imbeju kwa kudhamini mashindano ya mwaka huu ambayo sasa yanaingia msimu wake wa 13,” alisema Mkazuzu.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Ramadhan Shauritanga, ameahidi kusimamia mashindano hayo kwa uadilifu mkubwa na kwa kuzingatia sheria na kanuni zote za mchezo wa soka.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED