UJIO wa zaidi ya wageni 7,000 mkoani Iringa kwa ajili ya mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA), umeleta neema kubwa kwa wafanyabiashara wadogo, hususan waendesha bodaboda, mama na babalishe, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma mbalimbali.
Katika Manispaa ya Iringa, waendesha bodaboda wamesema idadi ya safari imeongezeka kwa kiasi kikubwa, huku wageni wakihitaji usafiri kwenda viwanja vya mashindano, maeneo ya malazi na sehemu za huduma.
Mmoja wa bodaboda, Evans Mmbando, amesema kabla ya mashindano alikuwa akipata safari chache kwa siku, lakini sasa kipato chake kimeongezeka kutokana na ongezeko la wateja.
“Tunaishukuru serikali kwa kuleta mashindano haya Iringa kwani yameongeza mzunguko wa fedha. Kwa sasa tunapata hadi Sh. 40,000 hadi 50,000 kwa siku,” amesema.
Kwa upande wake, Gervas Msukuma amewataka madereva wa bodaboda kuwa nadhifu na kuheshimu kazi yao, akisema bodaboda imekuwa chanzo kikubwa cha ajira na kipato kwa vijana wengi.
Katika sekta ya chakula, babalishe Godfrey Reter amesema biashara imeimarika kwa kiasi kikubwa, akilazimika kupika chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wageni na washiriki wa mashindano.
“Nimekuja Lugalo Sekondari kujitafutia kipato kwa kuuza chakula wakati wa mashindano haya,” amesema.
Aidha, biashara nyingine zilizonufaika ni hoteli, nyumba za kulala wageni, maduka, wauza vinywaji, saluni na huduma za fedha kwa njia ya simu.
Wananchi wa Iringa wamesema matukio makubwa kama UMITASHUMTA yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mkoa kwa kuongeza mzunguko wa fedha na kutoa fursa za biashara.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED