Serikali imewataka waimbaji wa muziki wa Injili nchini kujenga utamaduni wa kuwekeza na kuweka akiba kupitia mifuko ya uwekezaji ili kuhakikisha mapato wanayopata kutokana na kazi zao yanawanufaisha kwa muda mrefu na kuwapa usalama wa kifedha baada ya kipindi chao cha kufanya kazi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Muziki kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kelvin Stanslaus, wakati wa uzinduzi wa msimu wa pili wa East Africa Gospel Music Awards & Festival (EAGMA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Stanslaus alisema sekta ya muziki imeendelea kukua na kuwa chanzo muhimu cha ajira na maendeleo ya kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa wasanii kujifunza kuwekeza sehemu ya mapato yao na kuanzisha mifuko ya pamoja ya uwekezaji itakayowawezesha kujijengea mustakabali mzuri wa kifedha.
"Ni muhimu wasanii wajifunze utamaduni wa kuwekeza na kuweka akiba. Kipato wanachokipata leo kiwasaidie kujenga maisha yao ya kesho na kuwakinga dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye," alisema.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na waandaaji wa EAGMA kwa kuwa tuzo hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa Injili, kuhamasisha ubunifu na kuongeza ushindani miongoni mwa wasanii wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa East Africa Gospel Music Awards & Festival (EAGMA), Magreth Chacha, alisema maandalizi ya msimu wa pili wa tuzo hizo yameanza rasmi yakilenga kuinua hadhi ya muziki wa Injili na kutambua mchango wa watumishi wa Mungu wanaotumia muziki kuhubiri Injili katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema msimu huu unatarajiwa kushirikisha washiriki kutoka zaidi ya nchi saba za Afrika Mashariki, ukiwa na kaulimbiu ya "Kupokea na Kukabidhi Kijiti cha Uongozi," inayolenga kuhamasisha urithishwaji wa huduma kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Magreth alisema tofauti na msimu uliopita, mwaka huu kutakuwa na utoaji wa heshima maalumu kwa waasisi na vinara wa muziki wa Injili walioweka msingi wa huduma hiyo na kuandaa kizazi cha sasa cha wahudumu kupitia muziki.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya EAGMA na Meneja wa Wapo Radio, Machange Junior, alisema maandalizi yanaendelea vizuri huku maboresho mbalimbali yakifanyika ili kuongeza uwazi, ubora wa ushindani na ushiriki mpana wa wasanii kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mapendekezo ya washiriki yataanza kupokelewa Agosti 1, 2026, majina ya walioteuliwa yatatangazwa Septemba 20, 2026, huku kilele cha utoaji wa tuzo hizo kikitarajiwa kufanyika Novemba 14, 2026.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED