VITA HORMUZ: Kutikisa Afrika kwa njaa, ughali wa chakula

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:12 PM May 06 2026
Mbolea ya kukuzia ya CAAN + inayozalishwa kwa malighafi za fosfeti ya Minjingu mkoani Manyara.
PICHA/HABARI:KISUMA MAPUNDA
Mbolea ya kukuzia ya CAAN + inayozalishwa kwa malighafi za fosfeti ya Minjingu mkoani Manyara.

VITA vya Marekani, Israel na Iran, vinatajwa kuwaathiri moja kwa moja wakulima wa Tanzania na Afrika, kwa kukwamisha kupatikana mbolea inayopitia mlango bahari wa Hormuz nchini Iran ambao umefungwa.

Njia hiyo husafirisha takribani asilimia 17 ya mbolea yote ya Afrika inayoagizwa kutoka nchi za Ghuba.

Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inataja mbolea kuwa moja ya bidhaa zinazoongoza kuingizwa kwa wingi nchini ,ikigharimu takribani Dola za Marekani bilioni 1.6 kati ya mwaka 2020 hadi 2024. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, anaongezea kuwa msimu wa 2023/2024, Tanzania iliagiza tani 728,758 za mbolea ikilinganisha na tani 504,122, msimu wa 2020/2021. Huku matumizi ya pembejeo hiyo yakiongezeka kutoka tani 363,599 hadi 848,884.

Wazalishaji na waagizaji wa Tanzania wameathirika kwa kiwango kikubwa na vita vinavyoendelea, watalaamu wanasema, ni hali inayochochea hofu ya kuvuruga upatikanaji wa bidhaa hiyo, kuongezeka gharama za uzalishaji, pamoja na kupanda kwa bei za malighafi za urea ambayo ni pembejeo muhimu kwa wakulima.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Shirika la Biashara Duniani WTO), asilimia 31 ya mbolea inayotumika Tanzania hupitia mlango wa Hormuz, wakati asilimia 54 ya mbolea yote ya Sudan hutumia njia hiyo , asilimia 26 ya mbolea ya Kenya na asilimia 27 ya Uganda zote zinasafirishwa kupitia mlango bahari wa Hormuz. 

WTO inaongeza kuwa theluthi moja ya mbolea yote duniani sawa na tani milioni 16, zinapitia hapo na kueleza kuwa ni njia muhimu sana kwa uzalishaji wa chakula duniani na inayootegemewa kupatikana na kusambazwa mbolea za viwandani.

“Kufungwa, kushambuliwa kwa meli zinazojaribu kuvuka, kutozwa ada kubwa zile zilizoruhusiwa kupita kiasi cha Dola 2,000,000 sawa na Shilingi bilioni tano na mamlaka za Iran na mashambulizi ya makombora ya viwandasha gesi asilia katika nchi za Ghuba vimepunguza uzalishaji na usafirishaji wa mbolea.” Inasema WTO.

AFRIKA INAPOATHIRIKAI

Gesi asilia inayozalishwa katika eneo la Ghuba ni malighafi muhimu katika kutengeneza virutubisho vikuu vya naitrojeni (N), fosfeti (P/phosphorus), na potasiamu (K) vikijulikana kama mbolea ya NPK ambavyo ni virutubisho vinavyohitajika zaidi kukuza, kustawisha na kufanikisha mimea kuzaa kwa wingi.

WTO inaongeza kuwa mwaka 2024, asilimia 25 ya mbolea zote za naitrojeni zilisafirishwa kuingia Afrika kupitia mlango wa Hormuz. Mbolea hizi za naitrojenia za amonia, urea, Diammonium Phosphate (DAP) Monoammonium Phosphate (MAP) za kupandia zinazozalishwa kwa kutumia gesi asilia. Ndizo zinazotumika kwa wingi zaidi barani Afrika takribani asilimia 63 ya mbolea yote inayotumiwa kwa

mwaka.

Wazalishaji wakubwa wa mbolea Afrika wanategemea mali ghafi hizo kuzalishia mbolea wanazozisambaza katika mataifa mengine , mfano kampuni ya OCP ya Morocco inaagiza tani milioni 8.5 hadi tisa za salfa (sulphur) sawa na asilimia 48 kwa mwaka kutoka nchi za Ghuba ya Urabuni. Salfa inatumika kutengenezea mbolea za fosifeti, ammonia, DAP na MAP.

Afrika Kusini, kiwanda cha Richards Bay huzalisha zaidi ya tani 320,000 za mbolea za fosifeti na nyingine 210,000 za asidi ya fosforiki kila mwaka, kwa kuchakata mwamba wa fosfeti unaochimbwa katika mgodi wa Phalaborwa. Hata hivyo, hutegemea zaidi amonia na salfa kwa ajili ya shughuli hizo, ikiagizwa kutoka nchi za Ghuba.Takribani asilimia 87 ya amonia na asilimia 85 ya salfa vilitoka Mashariki ya Kati.

KILIO CHA AFRIKA 

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, anaeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali hiyo, akionya kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu yanavuruga minyororo muhimu ya usambazaji na yana athari kubwa kwa biashara kimataifa.

Athari za hali hiyo zinaonekana karibu Afrika nzima, mataifa ya Afrika Masharikina Kusini yanayopakana na Bahari ya Hindi hununua kati ya asilimia 30 hadi 50 ya mbolea zao kutoka nchi za Ghuba kupitia mlango Bahari wa Hormuz. Hali inayotishia mustakabali wa uzalishaji barani Afrika kutokana na uhaba na ughali wa mboleo utakaopunguza matumizi ya pembejeo hiyo.

Naye mchumi mwandamizi kutoka Oxford Economics Africa Leeuwner Esterhuysen, anasema katika taarifa za kimtandao: “Kwa sekta ya kilimo barani Afrika, hatari kubwa ni kupanda bei ya mbolea, kupunguza matumizi yake miongoni mwa wakulima, hususan wadogo wenye mitaji midogo. Hali hii inaweza kudhoofisha mavuno na afya ya mazao, na hivyo kuchangia kupungua kwa uzalishaji na kupanda kwa bei ya chakula kwa muda mrefu.”

Kwa wakulima wadogo katika nchi za Afrika Mashariki za Ethiopia, Kenya, Sudan, Somalia na Msumbiji, changamoto hiyo inamaanisha kupungua uwezo wa kumudu pembejeo muhimu, hususan mbolea za naitrojeni zinazochochea ukuaji na uzalishaji wa mazao katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

“Nimezunguka kwenye maduka kadhaa ya mawakala, lakini wengi hawana mbolea, na huku ndio msimu unachanganya nahitaji mbolea ya kukuzia lakini hazipatikani. Sijui itakuwaje,”Hilary Tesha, mkulima wa Hai, mkoani Kilimanjaro, anasema akinukuliwa na vyombo vya habari.

Kwa mkulima wa kawaida kama Hilary, hii siyo tu habari ya kimataifa bali ni hali inayogusa moja kwa moja mavuno yake, kipato chake, na usalama wa chakula kwa familia yake na jamii nzima. Kadri gharama zinavyoongezeka na upatikanaji kuwa mgumu, ndoto ya kupata mavuno mengi na bora inazidi kuwa changamoto kubwa kwa wengi.

“Nmekwenda kwenye ghala la NCPB, karibu mara kumi, natafuta mbolea ya urea, hakuna na mahindi yameshafika usawa wa magoti. Nina wasisi nisipopata mbolea kwa wakati, mahindi yangu yanaweza kuharibikia shambani,” anasema Judith Okango, mkulima kutoka kata ya Kwanza, mkoa wa Trans-Nzoia, Kenya.

Judith ni mmoja ya wakulima wengi wa eneo hilo waliokuwa wamekusanyika nje ya ghala la serikali ya NCPB (National Cereals and Produce Board) wakifuatilia upatikanaji wa mbolea katika kipindi hiki wanachohitaji kuweka mbolea ya kukuzia. Na hata kwa wale wanaopata hawapewi kiasi wanachohitaji.

Kwa upande wa mawakala wa pembejeo nao wanakumbana na changamoto ya uhaba wa mbolea za kukuzia katika msimu huu, kama anavyosema Ayubu Juma, muuzaji wa pembejeo za kilimo, mkoani Kilimanjaro:

Anasema mbolea ya kukuzia imekuwa shida, kwa mawakala wadogo na wakubwa pia.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Jimbo la North Dakota, Marekani kupitia kitengo chake cha Ufuatiliaji wa Biashara ya Kilimo (Agricultural Trade Monitor), unaonesha kuwa iwapo mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa hadi robo ya pili ya mwaka (Juni 2026), bei ya mbolea ya DAP inaweza kupanda zaidi ya Dola 800 (Sh 2,000,000) kwa tani kutoka dola 380 (1,000,000 ) mwaka 2025. Bei ya urea inakaribia kufikia kati ya dola 850 hadi 900 kwa tani sawa na Sh.milioni 2.3.

MWANDISHI WA MAKALA HII NI KISUMA MAPUNDA

Ni wakati wa viwanda vya ndani vinavyotumia fosfati ya Minjingu mkoani Babati yenye fosforasi na kalshamu zinazotumiwa na udongo kurutubisha mimea, kutumia fursa hiyo kujiimarisha kiuzalishaji.