Tanzania ina fursa za kuinua wananchi kiuchumi lakini mambo hayaendi. Upo ugonjwa unaotafuna juhudi hizo ni kukosa uaminifu, uadilifu na weledi kwa wale wanaopewa ruzuku, mikopo au mitaji ya kuanzisha miradi midogo na mikubwa.
“Watanzania tukumbuke kuwa mtaji mkuu kuliko mingine katika mambo yote ni hofu ya Mungu, uadilifu na uaminifu.Tanzania inakosa watu hawa,” anasema Samwel Mdachi Mkurugenzi waMafunzo, Utafiti na Ugani Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Anaeleza kuwa wanakosekana watu wenye sifa hizo, hata kama wapo ni wa kutafutwa au wachache mno, anatoa, mfano kuwa mjasiriamali anapokea fedha za mradi lakini hafanyi kazi au anachukua mkopo wa halimashauri anatoroka na fedha za serikali, haufanyii kazi wala harejeshi fedha ili wengine wanufaike.
Anafafanua zaidi, wanapewa mitaji, mafunzo, vifaa lakini hakuna maendeleo. Nchi inakosa watu waaminifu na weledi na waliokuwepo ni wachache au wa kutafuta. Anawataka wanaopokea au waliochukua rasilimali zikiwamo fedha, mafunzo na mitaji wajipime na kujihoji, upungufu huo utaendelea mpaka lini?
Anagusa miradi ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) kwenye uvuvi, ambayo serikali inatoa mitaji kuwekeza kwenye rasilimali za maji lakini vijana wanatorokana pesa au hawafanyi lolote kama ilivyokusudiwa.
Anaonya:“Kumbukeni serikali inatafuta fedha, inaandaa na kuwapatia vijana maeneo ya uwekezaji lakini hakuna matokeo badala ya kufanya bidii ufanikiwe unarudi nyuma wewe na taifa pia.”
Mdachi anazungumza hayo wakati akizindua Mtaala wa Kozi ya Mafunzo ya Uongozi wa Jamii wa Uhifadhi wa Rasilimali Bahari, pamoja na kukabidhi vyeti wakufunzi wa kwanza wa kozi hiyo, uliofanywa na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Mbegani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Mafunzo hayo yanalenga kuwafundisha wananchi na jamii za ukanda wa pwani na kuwashirikisha kulinda rasilimali za chini ya maji iwe baharini, mtoni, kwenye mabwawa na maziwani.
FETA kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi wa Asili (UICN) wamewafunza viongozi wa Vikundi vya Usimamizi wa Pwani (BMU) na Kamati za Uvuvi za Shehia (SFC) upande wa Pemba.
Mdachi anawaambia hayo, wahadhiri, wadau na wahitimu (wakufunzi) maofisa uvuvi naviongozi kutoka kisiwani Pemba na mkoa wa Tanga, ambao wameshiriki mafunzo hayo kwa majaribio kabla ya program kusambaa nchi nzima:
“Vijana wengi wanalaumu na kukosoa serikali lakini wajipime wana uaminifu, uadilifu na weledi? Maana ndicho kikubwa kinachokosekana kwa wengi sasa.Nimeona niliseme hili maana sehemu nyingi hatulizungumzii ni tatizo linaloathiri si tu maendeleo yao binafsi bali pia jamii nzima.”
Akigeukia mafunzo anawataka pia wahitimu hao 12 wanawake nane na wanaume wane kutoka Pemba na Tanga kuwa wamefundishwa watumie ujuzi na maarifa kwa weledi na uadilifu kwa sababu wamepewa utaalamu ambao ni rasimali.
Serikali inategemea mafunzo yatumiwe kutambua rasilimali na kuzilinda, kuwa viongozi bora, kudhibiti uharibifu, kufahamu na kutumia sheria na sera kusimamia jamii zitumie rasilimali za uvuvi na pwani kwa uendelevu, anasema.
Aidha, watumie mafunzo ya uongozi kushirikisha jamii na kuongeza: “Jambo la muhimu ni kutekeleza mafunzo kivitendo, kusimamia majukumu kwa weledi, kusimamia maadili, uwajibikaji katika maeneo mnayoyasimamia.”
Anataja kubadilika na kuwa na hofu ya Mungu, kutatua migogoro kwa amani, uwazi na kuhakikisha usahihi wa matumizi ya uwazi wa mapato na ushirikishaji ili kulinda rasilimali zinufaishe vizazi vya sasa na baadaye zaidi hata miaka 300.
Eva Msella ni Mratibu wa Ukanda wa Pwani (sea scapes) za Tanga na Pemba wa shirika la IUCN, linashiriki kutoa mafunzo hayo, anazungumzia uadilfu na uaminifu kwamba ili mradi huo ulete mabadiliko kusimamia rasilimali bahari, pwani na maliasili za uvuvi weledi na uaminifu havikwepeki.
“Wakufunzi wafanyekazi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na hofu ya Mungu ili kuwe na tija.Mafunzo ni mtaji, wahitimu wayatumie kusimamia rasilimali za uvuvi. Wanaokiuka sheria waadhibiwe, uharibifu udhibitiwe, yatatue migogoro, kuongeza mapato, kuleta mabadiliko na kuibua ubunifu wa kutumia rasilimali nyingine kupata mapato badala ya kutegemea zaidi viumbe wanaoishi majini,”anashauri Eva.
Eva anaongeza kuwa IUCN inatamani mafunzo yanayotolewa yalete uendelevu kwa manufaa ya sasa na miaka ijayo na yatumiwe kuondoa umaskini kwenye jamii yaibue fursa nyingine za kiujasiriamali pia kuongeza mapato ya serikali kuu na za mitaa.
Yatumike pia kufikia mikopo ya halmashauri na ile ya mfuko wa mitaji kujiendeleza kiuchumi na kubadili maisha ya wananchi wa ukanda wa Pwani.
Anaeleza kuwa haipendezi kusikika matatizo yanaendelea kuwepo au hayajatatuliwa na hali kubaki kama ilivyokuwa wakati mafunzo, ujuzi na rasilimali zimetumika na kazi zimefanyika kufunza viongozi.
Mtendaji Mkuu wa FETA Mbegani, Wakala wa Mafunzo ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, Dk.Semvua Mzighani, akawa na neno kuwa FETA pamoja na wadau, serikali na IUCN wana mpango wa kuyapeleka mafunzo hayo nchi nzima ili kuifundisha jamii kulinda na kuhifadhi rasilimali za uvuvi.
Anaongeza kuwa jukumu hilo ni utekelezaji wa lengo namba 14 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 14) linalohusu viumbe chini ya maji
Anakumbusha, linalenga kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu bahari, na rasilimali zinazopatikana ndani ya maji kwa maendeleo endelevu Anakumbusha kuwa serikali imewekeza kwenye miradi ya uvuvi wa vizimba, kupanda mwani, kunenepesha majongoo bahari kupitia BBT na uchumi wa bluu.
Aidha, Dk. Mzighani anataja bandari ya uvuvi Mtwara, iliyofikia asilimia 97 pamoja na uzinduzi wa meli kubwa ya uvuvi wa bahari kuu kuwa ni uwekezaji unaolenga kutumia rasilimali za majini kwa maendeleo ya kiuchumi na kuwataka wadau kushirikiana kuwafundisha Watanzania ili wafaidike na maliasili za uvuvi kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED