Tuambiane ukweli ni elimu bure au bila ada

By Rehema Matowo , Nipashe
Published at 03:14 PM Apr 21 2026
Tuambiene ukweli ni elimu bure au bila ada
Picha:Mtandao
Tuambiene ukweli ni elimu bure au bila ada

HIVI elimu ya Msingi nchini ni bure au ni elimu bila ada? Nimeanza na swali kwakuwa mjadala kuhusu elimu bure umeendelea kuchukua nafasi kubwa katika jamii na hata ndani ya Bunge, hususan wakati huu wa mijadala ya bajeti.

 Kauli ya Serikali kwamba elimu ya msingi hadi kidato cha nne inatolewa bila ada imekuwa faraja kwa wananchi wengi, hasa kwa familia zenye kipato cha chini na cha kati .
 
Hata hivyo, nyuma ya kauli hiyo kuna ukweli ambao mara nyingi hauzungumzwi wazi kwamba “bure” inayozungumzwa ni ada, si gharama zote za elimu.
 
Hapa ndipo mgongano unaanza, kwa kuwa wazazi wengi wanapoambiwa elimu ni bure, wanachukulia kwamba hawapaswi kugharamia chochote kinachohusiana na masomo ya watoto wao.
 
Matokeo yake, michango ya chakula, walimu wa ziada, ulinzi au hata mitihani inapopendekezwa shuleni, hukumbana na upinzani mkali.
 
Hoja ya wazazi huwa moja “Kwa nini tuchangie wakati Serikali imesema elimu ni bure?”
 
Sijui kama tunajiuliza kwa kina maana halisi ya elimu bora? Je, inawezekana kweli mtoto apate elimu bora bila uwekezaji wa ziada kutoka kwa mzazi?
 
Ukweli ni kwamba Serikali imepunguza mzigo mkubwa kwa kuondoa ada, lakini haijachukua nafasi ya mzazi katika majukumu yote ya malezi na elimu ya mtoto.
 
 Elimu si ada tu. Elimu ni pamoja na mazingira ya kujifunzia, lishe ya mwanafunzi, vifaa vya kujifunzia, na hata uwepo wa walimu wa kutosha.
 
Pamoja na wazazi kutolipa ada bado katika shule nyingi za kutwa, changamoto ya chakula imekuwa kubwa.
 
Shue nyingi za msingi hata Sekondari chakula cha mchana kimekuwa changamoto,wanakaa darasani kwa muda mrefu bila chakula na bahati mbaya wapo wengine wanatoka nyumbani hawajapata mlo wowote.
 
Tafiti nyingi zinaonyesha wazi kuwa lishe duni huathiri uwezo wa mtoto kujifunza, hapa ndipo mchango wa wazazi unapokuwa wa msingi.
 
 Lakini badala ya kuona hili kama uwekezaji kwa mtoto wao, baadhi ya wazazi huliona kama mzigo usio wa lazima.
 
Vivyo hivyo, suala la walimu wa mkataba au wa kujitolea limekuwa mjadala mwingine, ukweli ni kwamba bado kuna upungufu wa walimu katika baadhi ya shule.
 
Pale ambapo wazazi wanapochangia ili kupata walimu wa ziada, lengo si kuwafaidisha walimu bali kuwasaidia watoto wao kupata muda zaidi wa kujifunza ili kufaulu vizuri .
 
Kupinga mchango huo ni sawa na kukubali mtoto asipate msaada wa ziada anaouhitaji,hapa niseme wazi hata walimu hao wakiondolewa anaepata hasara sio mwalimu bali ni mtoto na familia yake.
 
Najua kwa sasa wazazi hawaoni changamoto hiyo, lakini watoto wengine wa shule binafsi watakapofaulu na wa kwao kufeli ndipo watakumbuka shuka wakati kumepambazuka.
 
Hoja nyingine inayojitokeza ni kuhusu mitihani ya mara kwa mara. Wapo wanaolalamika kuwa ni mzigo kwa mzazi, lakini ukweli ni kwamba mitihani hiyo huwasaidia walimu kupima uelewa wa wanafunzi mapema na kuchukua hatua kabla ya mitihani ya taifa.
 
 Ni sehemu ya kumjenga mtoto kitaaluma,na sio lengo wala njia ya kumuumiza mzazi.
 
Tatizo kubwa hapa si umaskini pekee, bali pia mtazamo.Ndiyo, hali ya maisha ni ngumu kwa wengi, lakini je, suluhisho ni kukataa kila aina ya mchango?
 
 Au ni kutafuta njia mbadala za kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata kile wanachostahili?
 
Wazazi wanapaswa kuelewa kuwa wao ni wadau wakuu wa elimu ya watoto wao. Serikali inaweza kuweka msingi, lakini ujenzi wa nyumba unahitaji juhudi za pamoja.
 
Tukiamua kujitoa kabisa, tunawaachia walimu mzigo mkubwa ambao wenyewe hawawezi, na mwisho wa siku anayeumia si mwalimu wala Serikali,maumivu haya yanabaki kwa mwananfunzi.
 
Ni muhimu pia kutambua kuwa walimu wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu lakini bado wanajitahidi kuhakikisha wanafunzi wanafaulu.
 
Wanapopendekeza michango fulani, mara nyingi wanakuwa wameona pengo fulani linalohitaji kuzibwa, kuwapinga bila kuwasikiliza ni kuvunja ushirikiano muhimu kati ya shule na mzazi.
 
Hii haimaanishi kwamba kila mchango ni sahihi au unapaswa kukubaliwa bila mjadala. La hasha.
 
 Uwajibikaji na uwazi  katika michango hiyo vinapaswa kuzingatiwa. Lakini kupinga kila kitu kwa kisingizio cha “elimu bure” ni kujidanganya.
 
Tukubali tukatae hakuna elimu bora isiyo na gharama. Ni wakati sasa kwa wazazi kubadili mtazamo badala ya kuangalia michango kama adhabu, waione kama uwekezaji.
 
Mtoto anayepata chakula shuleni, anasoma katika mazingira bora, na anapata msaada wa kutosha wa walimu ana nafasi kubwa ya kufaulu na kuwa na maisha bora baadaye.
 
Tusipofanya hivyo, tutakuwa tunajenga kizazi ambacho kimepata nafasi ya kusoma lakini hakijapata ubora wa elimu. Na hapo ndipo tutakapokuwa tumeshindwa kama jamii.
 
Ni laziba tukubali ukweli huu mchungu kuwa ada  inaweza kuwa bure, lakini elimu si bure, serikali inafanya kwa sehemu yake, sasa ni nafasi ya mzazi kutekeleza wajibu wako kwa faida ya baadae ya mtoto wako.
 
Tukikwepa, hatuiumizi Serikali. Tunamuumiza mtoto wetu na kuharibu mustakabali wake.Wazazi, chaguo ni letu,tuwekeze leo au tujutie kesho mambo yakiwa yameharibika.
 
Rehema Matowo,ni Mwandishi Mwandamizi mkoani Dodoma.
Kwa maoni au ushauri wasiliana naye kwa rehema3@gmail.com