KATIKA moyo wa Wilaya ya Kibiti, kuna ndoto inayochipuka kimya kimya ambayo imelenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Ndoto hii ina sura moja kuu yaani ujenzi wa soko la kisasa. Soko hili halitakuwa tu mahali pa kuuza na kununua bidhaa, bali itakuwa nguzo muhimu inayoweza kubadilisha maisha ya wengi na kufungua milango ya mafanikio mapya.
Kwa mtazamo wa maendeleo, soko hili litakuwa kichocheo cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, likileta pamoja watu wa rika zote chini ya lengo moja la ustawi hapa ndipo ushirikiano utaimarika, na maarifa yatashirikishwa, na hivyo kujenga jamii yenye mshikamano na mwelekeo chanya.
Aidha, uwepo wa miundombinu ya kisasa utaongeza ufanisi katika shughuli za biashara, kupunguza changamoto zilizopo kwa muda mrefu kama vile upotevu wa bidhaa na ukosefu wa maeneo bora ya kufanyia biashara.
Hii itawapa wafanyabiashara uhakika wa ukuaji endelevu na kuwahamasisha kupanua shughuli zao zaidi.
Kwa kutambua umuhimu wa hilo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri imetenga Sh milioni 145 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo ilikuwasaidia wafanyabishara kufanya shughuli zao sehemu salama na hiyo nikutokana na namna halmashauri inavyomthamini kila mfanyabiashara anayechangia katika kukuza pato la halmashauri na taifa kwa ujumla.
Soko hilo ambalo ujenzi wake umeanza mwaka huu linatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miezi mitatu na litaondoa changamoto ya wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika eneo ambalo sio rasmi.
Akizungumza na makala hii, Afisa biashara wa Halmashauri hiyo, Sadelick Kihongosi anasema kukamilika kwa soko hilo kutapunguza adha kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wakinyeshewa mvua na kupigwa na jua pindi wakiwa kwenye sehemu zao za biashara.
"Awali wafanyabiashara walijenga wenyewe vizimba vyao ambavyo sio imara hivyo mvua na jua vilikuwa changamoto kwao na kuathiri makusanyo ya ushuru," anaeleza.
Kihongosi ambaye pia ni msimamizi wa ujenzi wa soko hilo anasema kati ya wafanyabiashara 64 ni 15 pekee waliokuwa wakilipa ushuru kwa mwezi na makusanyo yalikuwa ni Sh 512,000
"Kwa makusanyo haya ni wazi kwa mwaka tulikuwa hatufikishi hata millioni moja na hii ni kutokana na wafanyabiashara hao kutumia fedha zao kuboreshea vizimba vya biashara lakini kutokana na maboresho haya tutakusanya zaidi ya milioni moja,"anasema
Anasema Halmashauri iliona changamoto hiyo na kuamua kutenga fedha kwa ajili ya soko hilo ambalo miundombinu yake itakuwa ya kisasa na rafiki kwa wafanyabiashara wakati wote.
Kwa mujibu wa Kihongosi soko hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 100 na kwamba kipaumbele zaidi kitatolewa kwa wale ambao walikuwepo hapo awali.
Kihongosi ambaye pia ni msimamizi wa ujenzi wa soko hilo anasema kati ya wafanyabiashara 64 ni 15 pekee waliokuwa wakilipa ushuru kwa mwezi na makusanyo yalikuwa ni Sh 512,000
"Kwa makusanyo haya ni wazi kabisa kwamba kwa mwaka tulikuwa hatufikishi hata millioni moja na hii ni kutokana na wafanyabiashara hao kutumia fedha zao kuboreshea vizimba vya biashara lakini kutokana na maboresho haya tutakusanya zaidi ya milioni moja,"anasema
Anasema Halmashauri iliona changamoto hiyo na kuamua kutenga fedha kwa ajili ya soko hilo ambalo miundombinu yake itakuwa ya kisasa na rafiki kwa wafanyabiashara wakati wote.
Kwa mujibu wa Kihongosi soko hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 100 na kwamba kipaumbele zaidi kitatolewa kwa wale ambao walikuwepo hapo awali.
Anaeleza kuwa ushuru soko litakapokamilika utakuwa ni Sh 20,000 na haitazidi 50,000 na ushuru huo haulengi kumuumiza mfanyabiashara bali pande zote mbili zifaidike.

"Halmashauri yetu imejipanga kuboresha miundombinu ya wafanyabiashara na haitarajii kumuumiza mfanyabiashara tutaweka ushuru rafiki kati ya shilingi 20,000 na haitazidi sh.50,000".anaeleza
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo,Shaweji Mkundi anaipongeza serikali kwa kuwakumbuka wafanyabiashara hao kwani ndicho kiungo muhimu katika kukuza uchumi wananchi.
Naye Jumanne Hassan,mfanyabiashara wa soko hilo amesema soko hilo litakuwa moja ya masoko bora zaidi hivyo kuwafanya waweze kutoa huduma bora na kukuza kipato chao.
"Soko letu halikuwa kwenye ubora, kwasasa tunawashukuru viongozi wa halmashauri kuona hilo na kuhakikisha wanatuwekea mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwasababu kwa sasa tutakuwa na uhakika na usalama wa mali zetu katika kipindi cha jua na mvua hatuta kuwa na wasiwasi,"anasema.
Anasema ombi lao kwa viongozi ni kuhakikisha wanaopewa kipaumbele kupata vizimba kwenye soko jipya ni wale waliokuwepo awali wakifanya biashara katika soko la zamani.
Asha Mkwizu, anayejishughulisha na uuzaji wa mboga mboga, anasema soko hilo litakuwa neema kwasababu wamechoka kukimbizana na mvua.
"Tumechoka kukimbizana na mvua,jua na wezi lakini tukipata soko lenye mpangilio mzuri, tutafanya biashara kwa utulivu na mapato yataongezeka," anasema.
Kwa upande wake Mama Lishe,Rahma Athumani ,anasema awali walikuwa wanakutana na changamoto nyingi zilizokuwa zinatokana na ukosefu wa miundombinu bora ya kufanyia biashara, hasa wakati wa mvua na ukosefu wa huduma muhimu kama maji na umeme.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukipika na kuuza kwenye mazingira yasiyo na miundombinu bora mvua ikinyesha wateja wanapungua na chakula kinaharibika haraka.
Ujenzi wa soko hili jipya utanisaidia kupata eneo safi, lenye maji na umeme wa uhakika ninaamini nitaongeza idadi ya wateja na kipato changu kitaongezeka kwa sababu watu watakuwa na uhakika wa usalama wa chakula."anasema Rahma.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibiti A, Said Ruambo, amemuomba mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo kukamilisha kwa wakati ili wafanyabiashara waweze kuendelea na shughuli zao za uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi, ambaye pia ni fundi wa mradi huo, Yasin Njopeka anaiomba serikali kusaidia ukamilishwaji wa mahitaji muhimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.
"Tunaomba ushirikiano wenu ili tuongeze nguvu ya kuweza kukidhi matakwa ya ukamilishaji wa mradi kwa muda na kama mnavyoona kwa sasa maandalizi ya kujenga uzio ili kulinda usalama wa raia wakati ujenzi ukiendelea," anasema Njopeka.
Kibiti ilivyokiinua kikundi cha wapiga debe
Kwa muda mrefu, kazi ya kupiga debe imekuwa ikitazamwa kwa jicho la shaka ikihusishwa na utovu wa nidhamu na matumizi ya dawa za kulevya. Lakini katika Wilaya ya Kibiti, simulizi hiyo imebadilika kabisa. Vijana wamechagua njia tofauti: kujipanga, kubadilika na kujenga maisha yenye heshima.
Katika kituo cha mabasi cha Kibiti, kelele za kuita abiria na pilikapilika za wasafiri zinaweza kuonekana kama kawaida,lakini nyuma ya pazia hilo kuna simulizi ya kuvutia ya vijana waliogeuza kazi ya kupiga debe kutoka taswira hasi hadi kuwa chanzo cha mafanikio na heshima katika jamii.
Niwazi vijana wakiamua wanaweza kuwa mfano mzuri kwa jamii, hasa kwa kuondoa dhana hasi kuwa wale wanaojishughulisha na kazi ya kupiga debe wengi wao ni watumiaji wa dawa za kulevya jambo ambalo si kweli.
Katika kuthibitisha hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani imekuwa mfano wa kuigwa, ikiwa ni eneo ambalo vijana wanaweza kujifunza kutoka kwa wapiga debe wanaofanya shughuli zao katika kituo cha mabasi wilayani humo, ambao wameamua kukataa vitendo viovu na kujikita katika kujiletea maendeleo pamoja na kujiweka mbali na wasiotaka kubadili tabia.
Vijana hao wanatoka katika kikundi cha Umoja wa Wasafirishaji Kibiti Terminal (UWAKITE), chenye jumla ya wanachama 20, nane kati yao ndio waanzilishi na ambao wamesajiliwa katika mfumo na wanajishughulisha katika stendi hiyo.
Akizungumzia mafanikio ya kikundi hicho, Katibu wa UWAKITE, Hamis Omari, anasema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2018 kikiwa na shughuli moja ya kupiga debe, lakini kilitambulika rasmi na kupata usajili kwa ngazi ya halmashauri mwaka 2024.
Anasema kupitia uvumilivu na kujituma kwao, katika mwaka wa fedha 2025/2026 wamefanikiwa kuomba na kupokea mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri kiasi cha Sh milioni 80, fedha zilizowawezesha kununua gari aina ya Costa kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Kibiti hadi Dar es Salaam.
"Mafanikio haya yametokana na kujituma kwetu pamoja na kila mwanachama kujua wajibu wake. Kila mwanachama anatakiwa kuzingatia sheria tulizojiwekea, ikiwemo kuacha matumizi ya dawa za kulevya, kwani matumizi yake hupunguza sifa ya kuaminiwa na kupata mikopo," anasema Omari.
Mbali na sheria hizo, wameweka motisha ya kifedha kwa wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya kwa kutenga Sh 100,000 kutoka kwenye mapato yao, hatua iliyowezesha vijana 11 kuachana na tabia hiyo.
"Hii zawadi tuliweka kwa waliokuwa tayari ndani ya kikundi, na ni wazi tumefanikiwa. Kwa yule aliyeshindwa, tuliamua kujitenga naye kwa kuwa hafai katika kikundi chetu," anasema.
Anasema katika kuhakikisha uimara wa kifedha, kila mwanachama huchangia Sh 30,000 kwa mwezi, huku kikundi kikiweka akiba ya Sh 50,000 kila siku. Hadi Machi mwaka huu, walikuwa na akiba ya Sh milioni 19, fedha zinazosaidia katika urejeshaji wa mkopo unaotakiwa kulipwa ndani ya miaka minne.
"Tunatakiwa kurejesha takribani Sh milioni 1.6 kwa mwezi, lakini tunaamini tutamaliza mapema kutokana na nidhamu yetu ya akiba, inayofikia zaidi ya Sh milioni tano kwa mwezi. Hii itatusaidia kuongeza gari lingine na kila mwanachama kumiliki nyumba yake," anasema.
Anaishukuru Halmashauri kwa kuwapatia mtaji huo ambao umekuwa chachu ya mabadiliko, ukionyesha kuwa hata kazi ndogo zinaweza kuwa mwanzo wa mafanikio makubwa.
Omari anatoa wito kwa wanawake kuachana na mila potofu na kujitokeza kujiunga na kikundi hicho ili waweze kukuza uchumi wao.
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 290, Kifungu cha 37A, asilimia mbili zimetengwa kwa watu wenye ulemavu, asilimia nne kwa vijana, na nyingine kwa vikundi vya wanawake.
Kwa wanufaika, mafanikio hayo yana maana kubwa zaidi ya fedha kwani ni heshima, mabadiliko ya maisha na matumaini mapya.
Mwanachama Jumanne Majemba anasema kabla ya kujiunga na UWAKITE alikuwa hana mwelekeo wa maisha.
"Nilikuwa napiga debe bila mpangilio, kipato hakikuwa cha uhakika, na muda mwingi nilikuwa napoteza. Mara nyingi nilitumia fedha hizo kununua bangi na pombe. Sasa nina nidhamu ya kazi na fedha, naweza kujitegemea na kusaidia familia yangu," anasema.
Kwa upande wake, Asha Mussa, mmoja wa wanawake walioshududia kikundi hicho kikiundwa anasema kikundi hicho kimeanza kama utani na wengi walidhani akitafika mbali lakini kwa maendeleo haya waliyonayo wamevunja ile dhana kuwa kazi hiyo ni ya wanaume pekee.
"Maendeleo yao yananivutia sana lakini naogopa kujiunga kwasababu umri wangu umeenda sana nawasihi mabinti ambao hawana kazi wajitokeze waje kufanya kazi na ili waweze kukuza uchumi wao na kuachana na biashara ambazo hazifai katika jamii,"anasema Asha
Anaongeza,"binti akifanya kazi kwa malengo na kujituma ni wazi kipato chake kitamsaidia kuanzisha biashara ndogondogo pamoja na kulipia ada za watoto wake kama anao au kusaidia familia yake,"
Naye Shaban Salum anasema kikundi hicho kimempa nafasi ya pili maishani.
"Nilikuwa nimepoteza mwelekeo, lakini sasa nimebadilika. Nimejenga heshima yangu, na familia yangu inanithamini tena," anasema.
Wanufaika hao wanasema siri ya mafanikio yao ni mshikamano, uwazi katika mapato na matumizi, pamoja na kufuata sheria walizojiwekea.
Mbali na manufaa binafsi, kikundi hicho kimechangia kupunguza uhalifu, kutoa ajira na kuhamasisha vijana wengine kujiunga katika shughuli halali za kiuchumi.
Omari anasema wana mpango wa kupanua biashara kwa kununua magari zaidi ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwaondoa katika mazingira hatarishi.
Akizungumzia mafanikio hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti, Maria Katemana, anasema vikundi vinavyotumia mikopo ya asilimia 10 kwa malengo sahihi ni nguzo ya maendeleo ya taifa.
"Serikali itaendelea kuviwezesha vikundi vinavyoonyesha uwajibikaji. Mikopo hii si ya anasa bali ni mtaji wa kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa," anasema.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya hiyo,
Johnmery Richard, anasema mafanikio ya UWAKITE yanaonyesha umuhimu wa vijana kuungana badala ya kufanya kazi kwa mtawanyiko.
Naye Kaimu Mratibu wa Mikopo Wilaya ya Kibiti, Mbilima Tungaraza, anasema kikundi hicho ni mfano bora kutokana na nidhamu yao ya marejesho na mipango ya baadaye.
"Tunajivunia kikundi hiki kwa sababu hakina usumbufu kwenye marejesho na tayari kimeanza kutoa ajira. Malengo yao ya kuwa na kampuni kubwa ya usafirishaji yatafungua fursa nyingi zaidi kwa vijana," anasema.
Anaeleza kwamba Halmashauri hiyo inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa vikundi kunufaika na zabuni za serikali kupitia mifumo ya ugavi na manunuzi.
Sasa UWAKITE si kikundi tu ni darasa la Maisha na ni ushahidi kwamba vijana wakiamua, wanaweza kubadili simulizi zao na kuwa suluhisho la changamoto za jamii badala ya kuwa sehemu ya tatizo.
Akizungumzia kuhusiana na miradi hiyo Mkurugezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Hanan Bafagih anasema mafanikio yanayoonekana kupitia ujenzi wa soko jipya pamoja na uwezeshaji wa vikundi vya vijana ni sehemu ya dhamira ya Halmashauri hiyo kuhakikisha wananchi wanapata mazingira bora ya kujikwamua kiuchumi.
Anasema ujenzi wa soko hilo la kisasa utakuwa suluhisho la changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara ikiwemo kufanya biashara mazingira yasiyo salama.
"Lengo letu ni kuhakikisha wafanyabiashara wa Kibiti wanafanya shughuli zao katika mazingira salama yenye hadhi na yanayowezesha kuongeza kipato chao na Halmashauri kwa ujumla, tunatambua mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Halmashauri na Taifa kwa ujumla," anaeleza Mkurugenzi.
Kadhalika anapongeza Vijana wa kikundi cha Umoja wa wasafirishaji Kibiti Terminal (UWAKITE) kwa kuonyesha mfano bora kwa matumizi sahihi ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri akisema kwamba hatua hiyo ya kuwekeza kwenye usafirishaji ni ushahidi kuwa Vijana wakipewa fursa wanawezakuwa chachu ya maendeleo.
"UWAKITE wameonyesha kuwa nidhamu mshikamano na uwajibikaji vinaweza kubadilisha maisha ya vijana na hii ni mfano mzuri kwa vikundi vingine kuiga ili kuondokana na utegemezi na vitendo visivyofaa kwenye jamii," anasema.
Mkurugenzi huyo ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Halmashauri utaendelea kuboresha miundombinu ya biashara kwaweka mazingira racking kwa wawekezaji wadogo wakati pamoja na kuviwezeaha hiking vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ili kuongeza fursa za kiuchumi katika Wilaya hiyo.
Bafagih anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda miradi ya Mendeleo na kuitumia kama nyenzo ya kuboresha maisha yao na vizazi vijavyo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED