Ripoti yaitaja Tanzania kushindwa kudhibiti matumizi ya tumbaku

By Sagini Hamis , Nipashe
Published at 12:16 PM Apr 09 2026
Mkurugenzi wa Jukwaa la Udhibiti wa Tumbaku nchini (TTCF), Lutgard Kagaruki.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Jukwaa la Udhibiti wa Tumbaku nchini (TTCF), Lutgard Kagaruki.

Ripoti ya Kipimo cha Uingiliaji wa Tumbaku kwenye Sera za Afya ya Umma (GTI) imeonesha kuwa Tanzania inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ushawishi wa kampuni za tumbaku katika utekelezaji wa sera hizo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepata alama 80 na kushika nafasi ya 89 kati ya nchi 100 zilizofanyiwa tathmini kuanzia Aprili 2023 hadi Machi 2025, hali inayoiweka katika kundi la nchi zenye hali mbaya zaidi duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Jukwaa la Udhibiti wa Tumbaku nchini (TTCF), Lutgard Kagaruki, anasema matokeo hayo yametokana na tathmini ya namna serikali ilivyoshughulikia tumbaku katika sera, maamuzi na utekelezaji wa mikakati ya afya ya umma nchini katika kipindi hicho.

Anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizochukua hatua za kisheria kudhibiti matumizi ya tumbaku kwa kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Tumbaku wa Shirika la Afya Duniani (WHO FCTC) tangu mwaka 2007.

Anasema kupitia mkataba huo, nchi wanachama zinapaswa kuweka na kusimamia sera madhubuti za kulinda afya ya umma dhidi ya madhara ya tumbaku, ikiwamo kuzuia ushawishi wa sekta ya tumbaku katika uamuzi wa kisera, hususani kupitia Kifungu cha 5.3.

"Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo, kumekuwapo na changamoto kubwa katika utekelezaji wa sheria na miongozo hiyo, hali inayochangia kuongezeka kwa matumizi ya tumbaku na athari zake kwa jamii," Lutgard anasema.

Anasema moja ya athari kubwa ni ongezeko la Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) kama saratani, magonjwa ya moyo na matatizo ya mfumo wa upumuaji, ambayo yanahusishwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya tumbaku.

Anasema kuwa mwenendo wa Tanzania si wa kuridhisha, hasa ukizingatia matakwa ya Kifungu cha 5.3 cha Mkataba wa Kimataifa wa Mfumo wa Kudhibiti Tumbaku (WHO FCTC), ambao nchi iliridhia tangu mwaka 2007.

“Tunajua kwamba mwaka 2025 uingiliaji wa tumbaku katika afya ya umma umeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka 2023, na matangazo ya bidhaa za tumbaku yameongezeka kwa kiwango cha juu, kinyume na makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania iliridhia,” anasema.

Ripoti hiyo ilitumia viashiria saba vikiwamo ushiriki wa sekta katika sera, shughuli za uwajibikaji wa kijamii, manufaa ya sekta, mikutano isiyo ya lazima, uwazi wa mawasiliano, mgongano wa maslahi na hatua za kuzuia ushawishi.

Aidha, kila eneo limepimwa kwa ushahidi wa sheria zilizoko, mawasiliano rasmi na uamuzi wa serikali kwa kuzingatia matakwa ya mkataba wa FCTC.

"Matokeo yanaonesha kuwa ucheleweshaji wa sheria madhubuti tangu mwaka 2017, pamoja na uwazi mdogo, mikutano yenye ushawishi, misaada ya CSR na motisha za biashara zilizochangia alama 80, zimethibitisha mifumo udhaifu katika kulinda sera za afya ya umma." alisisitiza.

Aidha, alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo imebainika kuwa, Kifungu cha 5.3 cha WHO FCTC kinazilazimisha nchi wanachama kulinda sera za afya za wananchi, hususani sera za udhibiti wa tumbaku, dhidi ya maslahi ya kibiashara na mengine binafsi ya sekta ya tumbaku.

Hata hivyo, kifungu hicho hakijatumika ipasavyo nchini, jambo linalotoa mwanya kwa tumbaku kuingilia sera na hivyo kuhatarisha juhudi za kudhibiti tumbaku na athari zake kwenye jamii.

Kadhalika, ripoti imebaini matukio mengi ya uingiliaji wa sekta ya tumbaku na kuonesha namna serikali inavyoendelea kuwa katika hatari ya kuathiriwa na ushawishi huo, hivyo kushindwa kuweka hatua madhubuti za kulinda afya ya umma.

Mfano uliotolewa ni tukio la Septemba 2024 ambapo kulisainiwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Japan Tobacco (JT), kwa uratibu wa Ubalozi wa Japan, kwa lengo la kusaidia jamii katika sekta za afya, elimu na maji.

Kadhalika, udhibiti wa matumizi ya tumbaku unaonekana kulegea, ambapo maeneo maalum ya uvutaji sigara yaliyoanzishwa mwaka 2021 na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) hayapo tena.

Ripoti inaonesha matumizi ya shisha na bidhaa nyingine za tumbaku yanaendelea bila udhibiti katika maeneo ya burudani kama baa, migahawa na hoteli kubwa.

MADHARA KATIKA JAMII

Ripoti hiyo inaonesha wazi kuwa ongezeko la matumizi ya tumbaku linakwenda sambamba na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Kimataifa wa Matumizi ya Tumbaku kwa Watu Wazima (GATS) wa mwaka 2018, asilimia 8.7 ya watu wazima nchini sawa na watu milioni 2.6, wanatumia tumbaku. Asilimia 14.6 ni wanaume na asilimia 3.2 ni wanawake.

Aidha, watu wazima wanaoathiriwa na moshi wa tumbaku wa wengine, ambapo asilimia 32.9 hukumbana nao maeneo ya kazi, asilimia 13.8 majumbani, asilimia 31.1 kwenye migahawa, asilimia 77.0 kwenye baa na asilimia 15.3 katika taasisi za elimu ya juu.

Kwa mwaka, matumizi ya tumbaku husababisha vifo takribani 21,800 nchini, huku gharama ya vifo vinavyohusiana na tumbaku imefikia Sh.  bilioni 337.

Kadhalika, gharama ya huduma za afya ni Sh. bilioni 110; hasara ya uzalishaji kazini Sh. bilioni 373; na jumla ya hasara za kijamii na kiuchumi ikiwa ni Sh. bilioni 820, sawa na asilimia 0.5 ya Pato la Taifa (GDP).

NINI KIFANYIKE

Ripoti inapendekeza hatua kadhaa zikiwamo kupunguza mawasiliano kati ya serikali na sekta ya tumbaku na kuhakikisha yanafanyika pale tu inapobidi na kwa uwazi zaidi.

Kadhalika, ripoti inapendekeza serikali ikatae ubia na makubaliano yasiyo ya lazima ili kupunguza ushawishi kwenye sera za afya ya umma nchini

Pia inapendekezwa kuharakishwa kwa sheria mpya inayokidhi matakwa ya WHO FCTC ili kuzuia migongano ya maslahi kwa viongozi wa umma na kupunguza mikutano na mawasiliano yasiyo ya lazima na kampuni za tumbaku.

Vilevile, serikali inashauriwa kupiga marufuku shughuli zote za CSR zinazofanywa na kampuni za tumbaku, sambamba na kuanzisha utaratibu wa viongozi kurekodi mawasiliano yote na kampuni hizo.

Hatua hiyo inayotajwa kulenga kufunga njia za ushawishi unaojificha kupitia misaada ya kijamii na mikutano rasmi.

Mapendekezo mengine ni kusitisha matangazo, promosheni na udhamini wote wa tumbaku kwa mujibu wa Kifungu cha 13 cha WHO FCTC, pamoja na kutungwa kwa kanuni za maadili kwa viongozi wa umma kuhusu namna ya kushughulika na sekta hiyo.