Pwani inavyojivunia ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:46 PM Jun 26 2026
Mkuu wa Mkoa ws Pwani Abubakar Kunenge.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa ws Pwani Abubakar Kunenge.

Zilongwa mbali, zitendwa mbali.” Kauli hii maarufu ukiisikia, bila shaka unajua uko mkoani Pwani, mkoa unaokusanya makabila mbalimbali yakiwemo Wazaramo, Wakwere, Wangindo, Wandengereko na Wamatumbi.

Kwa miaka ya nyuma, wengi walikuwa na mtazamo kwamba mtu akitoka Pwani anatoka katika jamii ya watu wavivu wasiopenda kufanya kazi, wanaopendelea ngoma za asili, kukaa barazani na vijiweni wakinywa kahawa.

Lakini sasa, “zilongwa zitendwa.” Taswira ya Mkoa wa Pwani imebadilika kwa kiasi kikubwa. Leo hii, Pwani ya chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge, imekuwa mfano wa maendeleo kupitia uwekezaji mkubwa wa viwanda, ukuaji wa mapato na mafanikio katika afua ya lishe.

Ni Pwani yenye wananchi 2,024,947, ambapo wanaume ni 998,616 na wanawake 1,026,331 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mkoa huo wenye wilaya saba na halmashauri tisa umeendelea kuonyesha ukuaji wa uchumi mwaka hadi mwaka. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, pato la mkoa liliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,461,198 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi bilioni 3,795,761 mwaka 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, anasema kwa sasa Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa kinara wa shughuli za uwekezaji nchini. Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za serikali katika kuboresha sera za uwekezaji pamoja na uimarishaji wa miundombinu wezeshi, ikiwemo ubora wa barabara, upatikanaji wa umeme wa uhakika, huduma za maji na uwepo wa bandari. 

Aidha, uwekezaji huo umechochewa na utaratibu wa kutenga maeneo maalumu ya kongani za viwanda sambamba na uwepo wa sera rafiki zinazovutia wawekezaji kuwekeza mkoani humo.

Kunenge anasema wastani wa pato la mtu mmoja mmoja katika Mkoa wa Pwani umeongezeka kutoka shilingi 1,709,278 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi 1,827,979 mwaka 2023, hali inayotokana na kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Anasema mkoa huo unaendelea kusimamia na kuimarisha sekta zinazochochea ukuaji wa uchumi, zikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.

Kuhusu suala la demokrasia na utawala bora, Kunenge anasema Mkoa wa Pwani unaendelea kuimarisha mifumo ya kiutawala pamoja na uwezo wa viongozi na watendaji wa mkoa na mamlaka za serikali za mitaa ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

  UKUSANYAJI WA MAPATO 

Kunenge anasema mkoa huo umeendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato hadi Machi 2026 umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 216.02 sawa na asilimia 113 .91 ya lengo kati ya hayo kodi za ndani zimekusanywa asilimia 128 nukta 67 ya lengo, kodi ya forodha imekusanya asilimia 102 nukta 92 ya lengo,Alisema hii inaonesha ongezeko kubwa la ufanisi katika usimamizi wa mapato. 

Aliongeza kuwa katika ngazi ya halmashauri mwaka 2025 - 2026, halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya shilingi bilioni 87.95 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19 nukta 74. kutoka mwaka 2024/2025. Hadi Machi 2026 ziifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 92.4 Sawa na asilimia 105 nukta 07 ya lengo, Makusanyo hayo yameufanya mkoa kushika nafasi ya kwanza kitaifa. 

“Mafaniko haya yamechangiwa na uboreshaji wa mifumo ya ukusanyaji na usimamizi bora wa vyanzo vya mapato na ushirikiano wa wananchi kwa ujumla”. Alisema Kunenge

 Viwanda,Uwekezaji na Biashara

TOLEO

Katika eneo hili Kunenge anasema kuwa Mkoa wa Pwani ni wa kimkakati katika kukuza sekta ya Viwanda na uwekezaji kutokana na uwepo wa huduma za msingi na kiuchumi ikiwepo reli ya TAZARA, reli ya kati naya mwendokasi (SGR) ambapo km 95 zipo ndani ya mkoa wa Pwani.

Pia anaeleza kwamba mkoa huo upo karibu na uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) km 33.91, bandari ya Dar es Salam km 37 pia miundombinu ya barabara inayounganisha na mikoa yote hapa nchini  jambo ambalo ni fursa ya kufika masoko ya kitaifa na kimataifa.

 Anasema uwepo wa umeme gridi ya Taifa na chanzo umeme bwawa la Mwalimu Nyerere ndani ya mkoa ambalo lina uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 ni fursa katika mkoa katika kukuza uchumi wa viwanda.

 Kadhalika anasema mkoa huo umepitiwa na bomba la gesi asilia katika wilaya ya Mkuranga na tayari viwanda nane vimeunganishwa na taratibu za kuunganisha viwanda vingine vutatu zinaendelea.

 Aidha anabainisha kwamba Serikali ina mpango wa kujenga bomba kuu la gesi kutoka kinyerezi jijini Dar es Salam hadi Chalinze ambao utaongeza ufanisi katika shughuli za viwanda kwenye kongani za TAMCO. Zegereni,Moderm, Sino Tan, Elsewed na kuibua shughuli mpya za kiuchumi katika Wilaya za Kibaha, Kisarawe, Chalinze na Bgamoyo.

 Sekta ya Viwanda

 Akizungumzia sekta hiyo Mkuu huyo wa Mkoa anasema kwamba idadi ya viwanda imengezeka na kwa ujumla mkoa una viwanda 1,722 ambavyo ni vikubwa, vya kati na vidog. Kati ya hivyo vikubwa na vya kati vipo 457 na tangu uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan idadi ya viwanda vikubwa vilivyoanzishwa ni 269.  

 Kunenge  anasema idadi ya viwanda katika mkoa huo inaendelea kuongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2021 kulikua na viwanda1,387 hadi mwezi machi mwaka huu  vimefikia 1,722.

 “Katika kipindi cha awamu ya sita jumla ya viwanda 335 vimejengwa ambapo 82 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na viwanda 8 vimeanzisha uzalishaji ndani ya siku 100 toka kuapishwa kwa Mhe Rais Samia".

 Pia ajira zimeongezeka kutoka 14,559 mwaka 2021 hadi 22,289 mwaka 2026 Pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 62,000”. anaeleza Kunenge

 Kadhalika anasema mkoa huo unajivunia kuwa na viwanda vikubwa zaidi ya 22 vyenye uwezo wa kipekee katika teknolojia ya mitaji iliyowekezwa, ufanisi wa mitambo, aina na kiasi cha bidhaa zinazozalishwa  na masoko yanayofikiwa. 

Anataja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni pamoja na kiwanda cha sukari Bagamoyo,shamba la samaki Tanlapia,viwanda vya dawa kairuki,Katwaza na Medeor, viwanda vya vioo Suphare na KEDA, kiwanda cha nguzo za umeme Cost Cocrete poles, Multcable,  Goodwill, Lodhia steel,machinjio za Tanchoice, Union meat na Hill Packaging. 

Pia kunenge anasema vipo viwanda vinasafirisha zaidi ya tani million 20 za bidhaa mbalimbali kwa mwaka, bidhaa hizo ni pamoja na dawa za binadamu,vigae, magari/malori na pikipiki yaliyounganishwa, sabuni, nondo, sukari, samaki, nyama, mifuko ya plastiki na chumvi.

 Anasema mkoa huo una maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda 34 yenye ukubwa wa ekari 116,718.39 ikiwa ni moja ya fursa zinazovutia uwekezaji katika mkoa huo.

 Sekta ya Biashara

 Kunenge anasema uchumi wa mkoa huo unaendelea kukua kwa haraka huku sekta ya biashara ikiwa ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa ikijumuisha bidhaa na huduma ikiwemo maduka ya reja reja, nyumba za kulala wageni na maduka ya dawa muhimu.

 Anasema biashara zimeendelea kukua kutoka 10,403 kwa mwaka 2021 hadi kufikia 36,699 machi 2026, na kwamba usajili wa wafanyabiashara wadogo unaendelea na hadi sasa wafanyabiashara 4,813 wamesajiliwa wakiwemo wanaume 1,507 na wanawake 3,306.

 Hali ya uwekezaji

 Mkuu wa Mkoa anasema fursa zilizopo katika mkoa huo zimewezesha miradi 166 kusajiliwa katika Kituo cha uwekezaji (TIC) kwa mwaka 2024 na kwamba miradi hiyo itaingiza mitaji yenye thamani ya dola za Kimarekani Milioni 1,243.87 na itazalisha ajira 49,784.

 Anasema kwa mwaka 2025 kipindi cha Januari hadi machi, 2026 miradi 48 imesajiliwa yenye zaidi ya thamani ya dola za Kimarekani Milioni 780.83 ambayo itazalisha ajira 10,938.

 Miradi ya Kimkakati

 Mkoa unaendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo mpango wa uendelezaji mji wa Kibiashara wa Kwala ambao unahusisha upangaji wa eneo jipya linalojumisha maeneo ya Halmashauri tatu za Kibaha,

Chalinze na Kisarawe lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,171.6 ili kuanzisha Mji wa Kibiashara wa Kwala.

 Ujenzi wa miradi mingine ndani ya mji wa Kwala inaendelea ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya huduma na Viwanda katika Kongani ya viwanda ya Sino Tan, uendelezaji wa eneo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ujenzi wa bandari Kavu pamoja na maeneo ya bandari kavu za Nchi za Kongo, Rwanda na Burundi upo katika hatua za awali.

 Anasema upo pia mradi wa Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC) ambaou unatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 9,800 kwenye Vijiji vya Zinga, Kiromo, Kondo, Pande na Mlingotini ambapo uhuishaji wa Mpango Kabambe (Master Plan) umekamilika.

 Anaeleza kwamba mradi huo utajumuisha maeneo ya ujenzi wa viwanda vya maunzo ya nje (export zone), ujenzi wa viwanda kwa mauzo ya ndani maalum kwa watanzania, eneo la Bandari,maeneo ya makazi,

 Uwanja wa Ndege, Bandari ya uvuvi, mji wa Kijani na mji wa Starehe na Burudani.

Kadhalika anasema ujenzi wa Bandari Kuu ya Mbegani na Bandari ndogo ya Bagamoyo, ambapo mradi utahusisha ujenzi wa gati ya abiria na eneo la majahazi kwa pamoja.

 Anataja fursa nyingine za Uwekezaji kuwa ni kwenye vivutio vya utalii vipatavyo 87 ikijumuisha Mbuga za wanyama, maeneo ya Kihistoria,misitu ya Asili, Fukwe za Bahari, Matumbawe na aina mbalimbali za samaki.

 Anasema ukanda wa bahari wenye urefu wa km 300 unaofaa kwa uwekezaji katika uchumi wa buluu kama kilimo cha Mwani, ufugaji na unepeshaji wa samaki, kaa na majongoo bahari, kilimo cha chumvi, uwekezaji katika nishati safi na miradi ya hifadhi ya Bahari;

 Akizungumzia sekta ya ujenzi anasema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la uboreshwaji wa miundombinu ikiwa ni pamoja ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami, changarawe, udongo, ujenzi wa makalvati na madaraja.

 Anasema mkoa huo una mtandao wa barabara wenye urefu wa km 6,564.15 ambapo Wakala wa Barabara

Tanzania (TANROADS) inasimamia km 1,510.58 na Wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) inasimamia km 5,053.57.

 Kunenge anawaita wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali hapa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika mkoa huo kutokana na namna walivyojipambanua kwa kuwa na maeneo ya uwekezaji yenye miundombinu wezeshi.