Mkuranga inavyojivunia mabadiliko sekta ya afya

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 01:36 PM Jun 25 2026
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Waziri Kombo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Waziri Kombo.

HALMASHAURI ya Wilaya Mkuranga ni kati ya Halmashauri tisa za mkoa wa Pwani ambayo inajivunia kujiimarisha kwenye kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya huduma za afya kusogeza karibu na wananchi.

Mkuranga kwasasa ina vituo vya Serikali vya kutolea huduma za afya 71 kati ya hivyo Hospitali ya Wilaya moja, vituo vya afya saba na zahanati 63 huku kukiwa na watumishi 533 kati ya 1,539 wanaohitajika.

Wanajivunia maboresho makubwa katika Hospitali ya Wilaya kupitia fedha za serikali kuu wadau na Halamashauri amazo ni zaidi ya sh Bilion 2.5 kwa ajili ya kuongeza majengo na ununuzi wa vifaa tiba.

Maboresho hayo kwenye hospitali yamesababisha kuoata cheti cha utoaji huduma bora kutoka wizarani huku maabara ikitambuliaka kimataifa .

Kwa mujibu wa mganga mkuu wa Halmashauri hiyo kwa sasa zipo huduma zinatolewa ambazo awali hazikuwepo zikiwemo za madaktari bingwa, huduma za ziada za kinywa na meno, huduma za fiziotherapia na za Tehama.

Anasema Hospitali hiyo inahudumia wananchi  200 hadi 300 kwa siku huku wanaojifungua idadi yao ikiwa ni 400 hadi 500 kwa mwezi wakitokea ndani na nje ya Wilaya hiyo.

Uwepo wa Hospitali hiyo ya wilaya umesaidia upanuzi na uboreshaji wa huduma za afya  huku kukiwa na upasuaji wa kibingwa hususani kwa akina mama na mazoezi ya tiba

huduma ambazo awali hazikuwepo.

Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga inajivunia uwepo wa Hospitali hiyo huduma nzuri zinazotolewa sambamba na mazingira mazuri ya kupata huduma za afya. 

Yapo mafanikio ambayo Hospitali hiyo inajivunia ikiwa ni pamoja na wageni kufika kwa ajili ya kujifunza, maabara yenye ithibati ya kimataifa na kuwa washindi wa pili wa mwaka 2025 kati ya Halmashauri 184. 

Katika uboreshaji wa huduma za afya Halmashauri hiyo pia imeweza kujenga kituo chja afya Mwandege kwa gharama ya Sh. Million 250  ambapo majengo husika yapo tayari yamekamilika kurahisisha huduma kwa wananchi wa maeneo hayo. 

Zahanati nyingine ambayo imejengwa ni ya Bupu kwa sh. Million 264.5 fedha kutoka serikali kuu na kwasasa ipo katika hatua ya umaliziaji . 

Sambamba na miradi hiyi pia Halmashauri imepokea sh. Million 262.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mwanambaya  huku ujenzi na ukarabati wa zahanati na nyumba za watumishi ukiendelea kwa gharama ya sh. billion 1.2.fedha za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/2026. 

UTOAJI WA MIKOPO 

Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imetoa mikopo ya asilimia kumi ya sh. Milion 976.2 katika kipindi cha mwaka 2024/2025. 

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Mwanamsile Dossi amesema kwasasa halki ya urejeshaji wa mikopo kwa makundi yote imebadilika tofauti na ilivyokuwa awali. 

Amesema vikundi vingi vimekuwa vikirejesha fedha kwa wakati na kwamba ofisi yake inaendelea kujidhatiti katika ufuatiliaji ili ambao hawajapata waweze kunufaika kupitia marejesho ya waliokopa. 

Dossi anasema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 vikundi vya vijana 26 kati ya 53 vya makundi mengine ya wanawake na watu wenye ulemavu ambao walipata sh. 668.4. 

Kadhalika  katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri hiyo inajivunia kutoa sh 2.2 Bilion kwa ajili ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu ambapo kati ya vikundi 155 vilivyonufaika 56 ni vijana. 

Kikundi cha Mkuranga terminal ni moja ya vikundi vilivyonufaika na mikopo ya Halmashauri ambacho kilipata sh. 82.2 Milion. 

Jumanne Omari ni Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye anasema katika utoaji wa mikopo Serikali inatakiwa kuangalia vijana wenye vigezo na kuwakopesha mmoja mmoja badala ya kupitia kwenye vikundi. 

Anasema wapo vijana tayari wanamiliki nyumba zao na wanahitaji mitaji kuinua biashara zao kuwapatia kwa kupitia vikundi wengi hazikidhi mahitaji na hivyo kuendelea kudumaa badala ya kukua. 

“Ninachoomba kwa serikali ifikirie hili wengi wanakwama kurejesha mikopo wanayokopa kutokana na kupata fedha kidogo ambayo haikidhi mahitaji lakini pia wengine wanakwamishwa na wanaojiunga nao kwenye kikundi kwakua si wote wenye biashara moja,”anaeleza. 

Anasema kikundi chao cha Vijana terminal wanaendelea na marekjesho kwa ukamilifu huku wakizidisha kiwango walichowekewa na hiyo inatokana na kuwa na lengo moja tofauti na vikundi vingine. 

Anaoomba pia idara ya mikopo kutoa elimu ya mikopo kwa wakopaji lakini pia wawe na ufuatiliaji kwa waliokopa ili marejesho yafanyike kwa wakati na wengine waweze kunufaika. 

TOLEO
UWEKEZAJI 

Katika eneo la uwekezaji Halmashauri ya Mkuranga inajivunia kuwa na kiwanda kikubwa cha vioo ambacho uwekezaji wake bidhaa zinazozalishwa hakuna katika mkoa mwingine hapa nchini. 

Kiwanda cha kuzalisha vioo cha KEDA ambacho uwekezaji wake umegharimu dola za kimarekani 369 Milion ambazo ni sawa na sh. 700 Bilion za kitanzania.

Meneja Biashara wa kiwanda hicho. 

Masoud Suleyman, anasema mradi huo wa kiwanda cha vioo kinazalisha tani 600 kwa siku huku asilimia 20 ikiuzwa ndani ya nchi na asilimia 80 soko likiwa Afrika Mashariki, nchi za kusini mwa Jangwa la sahara (Asia), Asia na Amerika ya Kusini. 

Uongozi wa kiwanda hicho unasema unajivunia kuwekeza Mkuranga kutokana na mazingira rafiki  sambamba na upatikanaji wa nishati safi ya gesi asilia. 

Masoud anasema kiwanda hicho ambacho kinajengwa kwa awamu mbili awamu ya kwanza ekari 70 tayari zimeendelezwa katika mradi huo hukui awamu ya pili inasubiri namna watakavyojipanga kujenga kiwanda kingine. 

Hadi sasa kiwanda hicho kimetoa ajira 500 za moja kwa moja na zisizo rasmi ya 1000. 

KEDA INAVYOSAIDIA JAMII 

Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga pamoja na kunufaika na kodi kutoka katika kiwanda hicho pia upo mchango unaotolewa kwenye jamii ikiwa ni pamoja na marumaru zilizogharimu sh. 9 Milion .katika shule ya sekondari Gongon. 

Pia kiwanda hicho kimejenga wa daraja la kisayani ambalo limegharimu sh.150 Milion pamoja na kuwanunulia wananchi eneo la kuzikia katika kijiji cha Msufini kidete. 

Wawekezaji wa kiwanda hicho wanaiomba Serikali kuwarekebishia barabara kwa kufanya upanuzi katika eneo la mlima kulungu ili kuwaondolea hasara ambayo imekuwa ikipatikana y ash. 30 Milion kwa mwezi gari linapodondoka na kusababisha uharibifu wa bidhaa. 

 Wameomba pia kuanzishwa kwa kituo cha huduma ambacho kitakuwa na taasisi zote wezeshi, kuondoa usumbufu uliopo sasa ambao unawalazimu kufuata huduma ya baadhi ya taasisi katika mkoa wa Dar es Salam. 

Masoud anasema Halmashauri hiyo inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi hivyo ni vema Serikali ikaona umuhimu wa kuanzisha kituo hicho. 

Kwasasa mkoa wa Pwani una viwanda vikubwa 71 vinavyouza bidhaa zake nje ya nchi ambapo zaidi ya tani Milion 20 za bidhaa husafirishwa kwa mwaka . 

Viwanda  hivyo pia vinaelezwa kutoa ajira za moja kwa moja 22,289 na zisizo za moja kwa moja 62,000. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Waziri Kombo akizungumzia kuhusiana na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuidhinisha fedha zinazotatua matatizo yazid wananchi. 

Kombo mbali ya kumshukuru Rais pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Watendaji wa idara zote kufanikisha maendeleo na kumuinua kiuchumi mwananchi wa Mkuranga. 

Amesema Mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo yamekuwa yakikuwa kila mwaka kutokana na ushirikiano uliopo baina ya watumishi wake na kwamba yamekuwa yakitumika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu.