Msomaji wangu, tunaendelea na mada zetu za Maisha Ndivyo Yalivyo tukiwamulika wakwe zetu. Lakini kabla ya yote, hebu kwanza nikumegee umuhimu wa mke, aina za wake na tabia zao.
Pengine mtu atajiuliza mke ni mtu gani? Ni mwanamke aliyeolewa. Leo kuna aina mbalimbali ya wanawake wanaojiita ni wake. Wale wanaoitwa Delila, wengineYezbeli, wengine Sara na wengine akina Rebeca.
Wake wa aina ya Ruthu ni wenye upendo, wavumilivu na wanaweza kuchukuliana na hali ya aina yoyote ile.
Wake wa aina ya Delila na Yezebeli ni wake wakorofi, ni watu wasiotaka kushuka hata kama wamekosa.
Hawa wanawachukia wakwe zao bila hata sababu yoyote ya msingi.
Wake wengi huwalaumu wakwe zao, huku wakati mwingine wakwe hao hawana tatizo ila ni wao wenye matatizo.
Wake wengi wana tabia mbaya kiujumla. Natumaini kuwa wewe siyo mwanamke mpumbavu anayetajwa kwenye maandiko ya Mungu. Mithali 14:1 “Kila
mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake, bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”.
Kama mke ndani ya nyumba unaweza kujenga msingi imara wa ndoa yako kwa kutumia hekima na maarifa. Inahitajika hekima ya Mungu kuujenga ulimwengu.
Na hauhitaji chochote ila hekima ya kujenga nyumba yako.
Kama mwanamke hautakiwi kuropoka ovyo, bali kuwa na hekima ya kuongea na uwe unashirikiana na kinywa chako kabla haujaongea chochote.
Kama utakuwa na hekima utaweza kumchunga simba, lakini kama hekima haimo kwenye kinywa chako, hata kondoo utashindwa kumchunga!
Najua wewe siyo mpumbavu, onyesha upendo wako kwa mama mkwe wako.Mtii mume wako kwani hiyo ni amri ya Mungu. Ukishindwa kumtii mume wako, naye hatakaa atii kile unachohitaji akufanyie.
Ukitaka kutunza nyumba yako, kuwa makini na kinywa chako. Ongea maneno ya hekima na ruhusu hofu ya Mungu ikuingie. Kumbuka neno ni kama yai bichi likidondoa hutaweza kuliokota likiwa zima.
Hivyo unapaswa kulichukulia kwa umakini mkubwa. Uwe makini kuongea juu ya familia ya mumeo kwa sababu watatumia maneno ya kinywa chako kukushambulia.
Najua wewe siyo mwanamke mpumbavu, wewe ni mwenye hekima unataka kujenga nyumba yako. Hivyo, utakuwa mwangalifu wakati unapoongea.
Na kwa kufanya hivyo utakuwa salama hata kama mumeo au wakwe zako au ndugu wa mumeo wamekukasirikia, kuwa na hekima. Badilisha tabia yakokwa kufunga mdomo wako.
Uwe mwangalifu usije ukajiandalia karatasi ya talaka kwa kufungua kinywa chako. Jifunze kunyamaza na Mungu atakuongoza.
Sasa tuone mambo mwanamke anayopaswa kufahamu kama mke. Kama unatamani kuishi maisha marefu nauendelee kuishi kwa amani kwenye ndoa yako, fahamu yafuatayo. Ni maelekezo unahitaji ili kuwa na faida ya kudumu.
Usitapuuze kwani yanaweza kubadilisha kabisa sura ya nyumba na ndoa yako.
Kwanza elewa kuwa mumeo ni mwanaume na siku zote ni tofauti na wewe. Vipo vitu mumeo anatamani uvijue. Anataka umtii, umheshimu, umpende na kumpa kipaumbele.
Mwanaume anataka umpende kutoka moyoni, upende vitu anavyopenda kuvifanya akiwa hayupo kazini. Pia, uwe mwaminifu, utunze siri zake, watoto wawe wasafi wakati wote na kula chakula kizuri. Anataka awe mtu wa kwanza katika maisha yako kama mama alivyo mtu wa kwanza katika maisha yako.
Kadhalika, na yeye atamfanya mama yake mzazi kuwa mtu wa kwanza kwenye maisha yake, hivyo atakutelekeza.
Jambo lingine la kufahamu kama mke ni kutambua kuwa mume wako ana wazazi. Wake wengi wanaishi kana kwamba waume zao walitokea mbinguni na kwamba hawana wazazi.
Usipokuwa makini watakushughulikia na wanaweza kufikia hatua ya kukutoa kwenye nyumba ya mtoto wao.
Kingine fahamu kuwa mumeo anawapenda wazazi wake. Kosa kubwa ambalo utalifanya katika maisha yako ni kufikiri kwamba mume wako hawapendi wazazi wake.
Uwe na hekima ya kuwapenda. Endapo utawachukia, utakuwa unachukia mafanikio ya ndoa yako. Kumbuka mama mkwe ndiye alikuwa rafiki wa kwanza wa mume wako.
Ni mwanamke wa kwanza kuwahi kumpenda katika maisha yake na bado anampenda.
Pia mumeo anataka uwapende wazazi wake.Hata kama wamekufanyia ubaya gani endelea kuwapenda kama wazazi wako. Zaidi wiki ijayo.
Tuma ujumbe 0715268581.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED