Makumbusho yalivyo chanzo cha maarifa na uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:15 PM May 18 2026
Nyumba ya jamii ya Wanyakyusa House, Kijiji Cha Makumbusho, Mikocheni, Kinondoni MC, Dar.
Picha:Maktaba
Nyumba ya jamii ya Wanyakyusa House, Kijiji Cha Makumbusho, Mikocheni, Kinondoni MC, Dar.

Mei 18 ya kila mwaka, ulimwengu huadhimisha siku ya makumbusho duniani, ikiwa ni siku muhimu iliyoasisiwa na Baraza la Kimataifa la Makumbusho yaani International Council of Museums (ICOM) mwaka 1977kwa mujibu wa sheria.

Maadhimisho hayo yalianzishwa kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua mchango wa makumbusho katika kuhifadhi historia, utamaduni wa jamii mbalimbali na elimu kuhusu maisha ya mwanadamu.

Sheria ya Makumbusho ya Taifa ya Tanzania (Sura ya 281), na Sheria ya Mambo ya Kale (Sura ya 333), Taasisi imepewa jukumu la kusimamia uhifadhi na maendeleo ya mali za kale kwa madhumuni ya kitamaduni, kijamii, kihistoria na kisayansi, sambamba na kuchangia uchumi wa taifa kupitia utalii wa mambo ya kale na mipango mingine ya maendeleo ya urithi wa taifa.

Kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Kale ya mwaka 2008 ya Tanzania inalenga kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni na maeneo ya kihistoria.

Pia Inasisitiza usimamizi na uhifadhi wa maeneo ya urithi, kuimarisha sheria zilizopo, kuendeleza utalii wa mambo ya kale kwa uchumi, na kulinda vumbuzi vya kiakiolojia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Vilevile katika ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 inasisitiza katika kukuza utalii wa kitamaduni kwa kuonesha utamaduni wa mtanzania kwa wageni kupitia matamasha, makumbusho na safari za kitamaduni ndani na nje ya nchi. 

Makumbusho huchukuliwa kama hazina ya kumbukumbu za mwanadamu, kwani huhifadhi mabaki ya kale, sanaa, nyaraka na vifaa vinavyoonesha maisha ya vizazi vilivyopita.

Kupitia makumbusho, jamii hupata fursa ya kujifunza chimbuko la utamaduni wao na kuelewa safari ya maendeleo ya mataifa yao.

Maadhimisho ya siku hii duniani hujumuisha shughuli mbalimbali kama ziara za makumbusho, maonesho ya sanaa, semina na programu za elimu kwa vijana.

Mbali na elimu, makumbusho pia ni chachu ya utalii na huchangia kukuza uchumi wa nchi kwa kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mantiki hiyo, makumbusho si kumbukumbu za zamani pekee, bali ni daraja linalounganisha historia, utamaduni na maendeleo ya sasa.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo na urithi mkubwa wa kihistoria unaohifadhiwa katika makumbusho mbalimbali.

Moja ya maeneo muhimu ni Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyopo katika Kijiji cha Mwitongo Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, mahali alipozaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa.

Makumbusho haya yanaonyesha maisha na uongozi wake kupitia zawadi alizopokea, vifaa alivyotumia na kumbukumbu za harakati za uhuru wa Tanganyika.

Eneo hili limekuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi, watafiti na watalii wanaotaka kujifunza historia ya taifa.

Aidha, jijini Dar es Salaam kuna Makumbusho Village, maarufu kama Kijiji cha Makumbusho, kinachoonesha maisha halisi ya Watanzania wa kale.

Hapa hupatikana zaidi ya nyumba 30 za asili katika mitindo ya Tembe, Msonge na Banda, pamoja na maonesho ya ngoma za jadi, vyakula vya asili na bidhaa za mikono.

Ziara katika eneo hili humpa mgeni nafasi ya kujifunza na kufurahia utofauti wa tamaduni za makabila mbalimbali ya Tanzania katika eneo moja.

Kwa ujumla, Siku ya Makumbusho Duniani ni ukumbusho kwamba kulinda makumbusho ni kulinda utambulisho na fahari ya taifa.

Kwa kutembelea na kuthamini makumbusho, tunahakikisha historia na utamaduni wetu vinaendelea kuishi na kufundisha vizazi vijavyo.