KWA miaka mingi, wanawake wa Tanzania wamebeba mzigo mkubwa wa kutafuta nishati ya kupikia kazi ya kukusanya kuni, ambayo mara nyingi imeonekana kama jukumu la kawaida la nyumbani, imekuwa ikiambatana na hatari nyingi zikiwemo ubakaji, vipigo, mauaji, magonjwa na kupoteza muda wa kufanya shughuli za maendeleo.
Katika vijiji vingi vya Mkoa wa Mwanza, wanawake na watoto wa kike walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta kuni safari hizo zilikuwa chanzo cha hofu kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyokuwa vikitokea porini au maeneo ya mashambani.
Grace Shawishi mkazi wa Igudija 'B' Kusini Majengo Mapya kata ya Kisesa wilayani Magu anasema maisha ya wanawake wengi yamekuwa ya mateso kutokana na utegemezi wa kuni.
"Kwa siku unaweza kwenda kutafuta kuni mara mbili tunakutana na changamoto nyingi sana hasa nyakati za jioni ikiwemo kubakwa na kukimbizwa hovyo porini," anasema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kisha katika Kijiji cha Kitumba, Fikili Sengasenga, anayesema zamani ilikuwa kawaida kupokea taarifa za wanawake kubakwa au kushambuliwa walipokuwa wakitafuta kuni.
"Kipindi cha nyuma ilikuwa vigumu kupita mwezi bila kupokea taarifa za mtu kubakwa au kukimbizwa huko porini, lakini sasa hali imeanza kubadilika," anasema.
Mbali na ukatili wa kijinsia, matumizi ya kuni yamekuwa yakihatarisha afya za wanawake kutokana na moshi unaozalishwa wakati wa kupika.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 3.2 duniani hufariki kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba unaotokana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa wanawake na watoto ndio waathirika wakuu kutokana na muda mwingi wanaoutumia karibu na majiko.
Utafiti wa UN Women Tanzania wa mwaka 2023 unaonyesha kuwa wanawake wa vijijini walikuwa wakitumia saa tatu hadi nne kila siku kukusanya kuni na kupika. Kupitia matumizi ya majiko yenye ufanisi wa nishati, muda huo umepungua hadi chini ya saa moja, hali inayowawezesha kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kutambua changamoto hizo, Serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024-2034 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Deusdedit Malulu, anasema Mkoa wa Mwanza pekee umepokea majiko 19,530 kwa bei ya ruzuku ili kuongeza matumizi ya nishati safi.
"Ruzuku tuliyotoa mkoani Mwanza imefikia zaidi ya shilingi milioni 400 lengo ni kuokoa maisha ya wanawake, kuboresha afya zao na kulinda mazingira," anasema.
Hata hivyo, changamoto ya gharama za kujazia gesi bado ni kikwazo kwa baadhi ya wananchi Semeni Kasori mkazi wa Ihayabuyaga wilayani Magu anasema pamoja na manufaa ya gesi, gharama za kuijaza bado ni kubwa kwa kaya nyingi.
"Ninapika kwa haraka sana kwa kutumia gesi lakini ikisha kujaza ni gharama kubwa serikali ione namna ya kupunguza gharama ili watu wengi waweze kuitumia," anasema.
Licha ya changamoto hizo, ushuhuda kutoka kwa wanawake mbalimbali unaonyesha kuwa matumizi ya nishati safi yanaanza kuleta mapinduzi makubwa katika usalama, afya na ustawi wa wanawake nchini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED