Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inavyogusa maisha ya wananchi kupitia mapato ya ndani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:11 PM Jun 23 2026
Jengo la Halmashauri ya Kibaha.
Picha: Mpigapicha Wetu
Jengo la Halmashauri ya Kibaha.

WAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ni kati ya wanufaika wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa pasipo kuwabebesha mzigo wa michango, na hiyo ni baada ya Halmashauri kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka Shilingi Bilioni 7 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Bilioni 18 mwaka 2025/2026.

Ongezeko hilo la mapato limeiwezesha Manispaa ya Kibaha kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, ujenzi wa miundombinu na kuwaondolea wananchi changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.
 
 Akizungumza na Nipashe Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk. Rogers Shemwele kwa anaeleza kwamba katika sekta ya miundombinu, kwa mwaka wa Fedha 2025/2026 imetoa jumla ya Shilingi milioni 420 kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika kata 14, ambapo kila kata imepatiwa Shilingi milioni 30.
 
 Amesema, Halmashauri imeboresha vivuko mbalimbali vilivyokuwa kero kwa wananchi, hali iliyosaidia kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa manispaa hiyo.
 
 Kwa upande wa elimu Dk Shemwelekwa anasema shilingi milioni 900 zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 41 kwa ambavyo vitapunguza changamoto ya upungufu uliokuwepo hapo awali, tayari vyumba hivyo vimekamilika na vinatumika, jambo lililoboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
 
 Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetumia zaidi ya Shilingi milioni 400 kutengeneza madawati 4,000 yenye viti na meza 2,000 kwa shule za sekondari pamoja na madawati 2,00kwa shule za msingi, hatua iliyosaidia kupunguza uhaba wa samani mashuleni.
 
 Katika kuimarisha elimu bora, manispaa hiyo pia imejenga shule mbili za mchepuo wa kiingereza ambazo ni shule ya Mwambisi na Shule ya Mwalimu Nyerere, ambapo zote zimekamilika na tayari zinatoa huduma kwa wananchi.
 
 Akizungumzia upande wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu anasema Manispaa ya Kibaha imefanya uchunguzi na kubaini kuwa kundi kubwa la wajasiriamali lilikuwa halina mitaji ya kuendesha biashara zao na hata waliyonayo ilikuwa haikidhi mahitaji.
 
 “Kufuatia hali hiyo, halmashauri ilitoa elimu na kuhamasisha wananchi kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo na  zaidi ya shilingi bilioni 2.1 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kukuza biashara zao, hali ambayo imeongeza kipato kwa wananchi wengi na kuwafanya kuishukuru serikali kwa kuwajali.
 
 Dk.Shwemwelekwa amesema halmashauri hiyo itaendelea kuhakikisha wananchi wanafurahia uwepo wa serikali inayowajali na kusikiliza mahitaji yao.
 
 Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, manispaa imeweka mikakati ya kuendelea kuboresha barabara kwa kuongeza fedha za maendeleo hadi shilingi milioni 50 kwa kila kata kutoka katika mapato ya ndani, pamoja na kuongeza utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kukuza uchumi wa wananchi.
 
 Kwa ujumla, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeendelea kuwa mfano wa matumizi bora ya mapato ya ndani kwa kuwekeza katika miradi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
 
 Dk.Shemwelekwa anasema lengo la Serikali ni kutoa tabasamu kwa wananchi hivyo amewataka wananchi kulinda miundombinu hiyo na kuwataka kuendelea kulipa tozo mbalimbali za Manispaa kibaha kwa kuwa fedha hizi huwarudi wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
 
 HOSPITALI YA MANISPAA YA KIBAHA LULANZI ILIVYOLETA TABASAMU KWA WANANCHI
 
Wananchi wa Kibaha wameendelea kushuhudia maboresho makubwa katika sekta ya afya baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi ya afya inayogusa moja kwa moja maisha yao.
 
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Lulanzi Dk.Abdulkadri Sultan anasema uwepo wa hospitali hiyo umepunguza msongamano katika Kituo cha afya mkoani pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.
 
 
Dk Sultan anaishukuru Serikali ya awamu ya sita pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kuwekeza fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo na kufanya maboresho yanayopanua wigo wa kupokea wagonjwa wengi zaidi.
 
Anasema wakati hospitali hiyo inajengwa ilikuwa na wodi saba pekee lakini sasa zimefikia 12 huku kukijengwa kichomea taka ambacho awali hakikuwepo.
 
Sambamba na hilo Dk Sultani anasema awali walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji ambayo Manispaa hiyo imeitatua kwa kutenga sh. Milion 60 zilezoweka uhakika wa maji muda wote katika Hospitali hiyo.
 
“Mkurugenzi wa Manispaa Dk. Rogers Shemwelekwa ni kati ya kiongozi bora ambaye anaangalia changamoto na kuzitafutia utatuzi wa haraka kuleta tabasamu kwa wananchi na hili limeonekana kwa Hospitali yetu, ameweza kumaliza tatizo la maji ambali lilikuwa likilalamikiwa na wananchi wanaofika kutibiwa hapa;
 
“Tofauti na ilivyo awali bajeti ya afya katika hospitali yetu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku , Mkurugenzi ukimueleza changamoto anaishughulikia kwa haraka kwa kutafuta fungu ili mradi wananchi wakija kupata huduma hapa kusiwe na kikwazo na sisi tunaahidi kufanya kazi kwa weledi katika utoaji huduma uliobora unaozingatia weledi na maadili ya kazi zetu,”anasema.

TOLEO MAALAM MKOA WA PWANI
 
Anasema Mkurugenzi huyo ameendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya afya hususani katika Hospitali hiyo ambapo zaidi ya Milioni 480 za mapato ya ndani zimetolewa kuboresha hospitali huku katika bajeti ya mwaka 2026/2027 Manispaa hiyo ikitenga fedha kwa ajili ya uzio na njia za ndani ya Hospitali.
 
Pia anasema hospitali hiyo kwa sasa imefanikiwa kununua jenereta kubwa la KV 110 lililonunuliwa kwa Sh. Milioni 64 mapato ya ndani ya hospitali ili kuweza kuwa na umeme wa uhakika tofauti na lililokuwa awali lenye ukubwa wa KV 60.
 
“Pamoja na nguvu tunayopata kutoka serikali kuu na Manispaa na kuleta mabadiliko kwenye hospitali yetu tumetumia mapato yetu ya ndani na kununua jenereta kubwa hakunashida tena ya umeme, awali tulikuwa na jenereta moja na sasa tunayo mawili,” anasema.
 
Kadhalika anasema kwa sasa kipo chumba cha kuhifadhia maiti ambacho awali kilikuwepo lakini hakikuwa kinafanya kazi ila kwasasa kutokana na kutengenezwa vizuri na kuwekwa mahitaji yake wananchi wamepata sehemu ya karibu ya kuhifadhia miili ya ndugu zao.
 
Dk. Sultan anasema maboresho makubwa yaliyofanyika katika hospitali hiyo pamoja na huduma bora kutoka kwa madaktari wenye weledi yamechangia ongezeko la akina mama wanaofika kujifungua.
 
Anasema katika mwaka 2024/2025 wanawake waliokuwa wakifika kujifungua katika hospitali hiyo walikuwa 70 kwa mwezi na kwa mwaka 2025/2026 idadi imeongezeka na kufikia 250 ikichangiwa na wanaotoka wilaya za Mkoa wa Dar es Salam.
 
Mganga Mfawidhi huyo anawapongeza wakazi wa Picha ya Ndege na shule mbalimbali kwa kuhamasika na kuwa mstari wa mbele katika uchangiaji wa damu na kuifanya kuwa na akiba ambayo inawasaidia wahitaji.
 
“Upatikanaji wa damu ya uhakika katika hospitali yetu umechangiwa na mwamko wa wakazi wa Manispaa yetu ya Kibaha, na uhamasishaji tunaoufanya kwenye shule za sekondari umesaidia kupata wachangiaji, hapa kwetu mgonjwa akihitaji damu hakuna kusubiri kuleta ndugu damu ipo na atahudumiwa kwa haraka kuokoa maisha yake,” anasema.
 
Dk. Sultan anasema pamoja na Serikali kuendelea kufanya maboresho katika hospitali hiyo pia wapo wadau kutoka Korea wameanza ujenzi wa jengo (wodi) la watoto wachanga kwa gharama ya sh. 480 na kwamba tayari sh. Milion 250 zimetolewa.
 
Sambamba na hilo pia taasisi ya Uturuki inaendelea na ujenzi wa kisima cha maji pamoja na pampu ambachokitahifadhia maji lita 30,000 na kuwasaidia ndugu na wagonjwa wanaofika kupata huduma katika hospitali hiyo.
 
Ongezeko la watumishi katika hospitali hiyo pia linatajwa kuwa eneo ambalo litakwenda kuboresha hospitali hiyo ambapo Serikali imepeleka watumishi wapya 26 na wanaategemea kupata ongezeko zaidi la madaktari, wauguzi, afisa afya na wauguzi.
 
Dk. Sultan anasema wana makakati wa kuanza ujenzi wa majengo ya kusubiria wagonjwa kwa kutumia fedha za mapato ya hospitali sambamba na kuhakikisha wnapata mtandao wa uhakika kutoka mkongo wa Taifa ili kurahisisha huduma za matibabu kupitia mfumo ulioboreshwa.
 
Anasema upo pia mradi wa TACTIC unaotekelezwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijiini (TARURA) ambao utawezesha ujenzi wa barabara ya lami hadi Hospitalini hapo.
 
Miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa Zahanati mpya ya kisasa ya Kilimahewa iliyopo Mtaa wa Tangini, Kata ya Pangani, mradi ambao umeleta matumaini mapya kwa wakazi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
 
Aidha, kiasi cha sh. Milioni 233.5 za mapato ya ndani kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa zahanati mpya moja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya karibu yake.
 
Wananchi wa eneo hilo sasa wanapata huduma za afya karibu na makazi yao, hatua itakayopunguza gharama za usafiri, msongamano katika vituo vikubwa vya afya pamoja na kucheleweshwa kwa huduma za matibabu.
 
Katika kuendelea kuimarisha huduma za afya, Manispaa ya Kibaha imetumia shilingi milioni 521.1 za mapato ya ndani kwa ajili ya Ujenzi wa kituo cha Afya Kongowe, sambamba na ukarabati, ukamilishaji na ujenzi wa miundombinu ya afya ikiwemo Wodi 6 na majengo ya OPD 5 katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.
 
Hatua hiyo inaonyesha namna mapato ya ndani yanavyoendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi wa Kibaha, huku ikiwa miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele kwa lengo la kuboresha ustawi wa jamii. 

 
 MAPATO YA NDANI YALIVYOGEUKA MKOMBOZI KIKUNDI CHA LULU YA WAJANE
 
Kikundi cha Lulu ya Wajane chenye wanachama watano kilichopo Kongowe kinatajwa kuwa kikundi bora kuwahi kutokea kutokana na namna kilivyosimamia weledi katika kurejesha mikopo waliyochukua kwenye Halmashauri hiyo.


 Nipashe ilipata nafasi ya kukutana na wanachama ambao walimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kwa kuwa nao karibu katika kila hatua na kufanikisha malengo waliyojiwekea ikiwa kumaliza mkopo kabla ya muda.


 Kanyenda Mweri ni Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye anaeleza kwamba walianza mwaka 2022 wakiwa wanakikundi watano na kujichangisha kila mmoja sh. Milion tano kwa ajili ya kuanza shughuli ya kufuga kuku.


 Anasema kwamba lengo lao ilikuwa ni kutambuana, kusaidiana, kutatua changamoto na kutumia fursa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi endelevu sambamba na kusaidia makundi maalumu.


 Mweri anasema kwa mara ya kwanza mwaka 2025 waliomba mkopo wa sh. Million 92  na kupatiwa sh. Million 46 ambayo walitakiwa kuirejesha ndani ya miezi 36 na walimaliza katika kipindi cha miezi 11 na kuomba tena sh. Million 250.
 
 Anasema kupitia ufugaji wao wa kuku wanaowauza kwa bei ya reja reja na jumla wameweza kupata mafanikio makubwa ambayo yamewasukuma kuomba mkopo mkubwa zaidi ili wainue ujasiriamali wao.
 
 Anasema katika awamu ya pili waliyoomba mkopo huo waliidhinishiwa sh. Milion 150 ambayo wameahidi kuisimamia kufikia malengo waliyojiwekea na kukamilisha urejeshaji wa mkopo huo kwa wakati uliopangwa.
 
 “Katika awamu hii ya pili tunakwenda kuanza mradi wa minofu, mashine ya kutotoreshea vifaranga na mashine ya kutengenezea chakula cha kuku na tukifanikiwa katika haya mradi wetu wa kuku utazidi kutuinua kiuchumi na kikundi bora kinachonufaika na mikopo,” anasema.
 
 Anasema kikundi hicho pia kimefungua kimezalisha kikundi kingine cha Lulu ya wajane inayojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na nazi na hiyo imetokana na maombi ya walio wengi kutaka na kujiunga na kikundi hicho.
 
 “Wengi waliona tunachofanya na wanataka kujiunga sasa sisi tulijadili hili na kufikia maamuzi ya kuanzisha kikundi kingine chenye wanachama watano ambacho kitajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na nazi tu, lengo letu mjane aweze kuinuka kiuchumia tutaangalia hapo baadae kuzalisha Lulu ya wajane wengine na bidhaa watakayojishughulisha nayo,” anasema
 
 Katibu wa kikundi hicho Rehema Mwaruka anasema awalai hawakuwa na watalaamu wa mifugo katika kikundi chao lakini sasa wameweza kuajiri vijana wawili ambao wanasimamia kukuhao na kuwatibu kwa wakati pale yanapotokea magonjwa.
 
 Rehema anaipongeza Manispaa kwa utoaji huo wa mikopo ambayo imekuwa ikifuata taratibu na kutolewa kwa weledi hali iliyowafanya walio wengi kuendelea kuinuka na kujipambanua kiuchumi tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuomba mikopo hiyo.
 
 Wanachama wa kikundi hicho Kayenda Mweri, Rehema Mwaruka, Mwajuma Tyea, Praxeda Kizinga na Pili Shija wameishukuru Halmashauri kwa namna inavyokuwa nao karibu kiuwashauri katika ujasiriamali wao sambamba na kuwapatia mikopo na kuahidi kuwapatia fremu katika soko jipya linalojengwa eneo la Loliondo kwa ajili ya kuuzia bidhaa zao.
 
 Hali kadhalika kijana Christopher Asenga (33) mkazi wa Muheza kata ya Mailimoja anaishukuru Halmashauri kwa namna ilivyomsaidia kutoka kwenye hali duni ya kimaisha na kumuwezesha kupata mkopo alionunulia bajaji ambayo inamuingizia kipato.


 Asenga anasema kabla ya kunufaika na mkopo huo maisha yake yalikuwa yakimtegemea baba yake ambaye hata mlo wa siku ilikuwa ni changamoto na kupitia mkopo huo kwasasa ana uhakika wa chakula huku akiendelea kurejesha na kuweka akiba.


 Katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa mikopo yenye thamani y ash. Bilion 2.160 kwa vikundi 457 vikiwemo vya vijana 161, Wanawake 275 na wenye ulemavu 21.
 
 SHOPPING MALL MRADI UNAOINGIZIA MANISPAA ZAIDI YA MILION 400 KWA MWAKA


 Afisa Uwekezaji na Viwanda wa Manispaa ya Kibaha Maryciana Deus anaelezea mradi wa shopping mall ambavyo umeendelea kuwa sehemu ya kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo na kufikia kukusanya sh. Milion 404 kwa mwaka.


 Anasema mradi huo ambao uwekezaji wake ni wa Bilion nane kwasasa una wapangaji 71 ambao wanatoka ndani na nje ya Manispaa ya Kibaha.
 
  Maryciana anasema pamoja kuwa kwasasa wanaendelea na matangazo kwa wakazi wa Kibaha hadi Dar es Salam kutangaza bidhaa zinazopatikana katika duka hilo la kisasaa huku wakijivunia muitikio unaoendelea kupatikana.
 
 Akizungumzia kuhusiana na kuwarahisishia usafiri wananchi waweze kufika kwenye duka hilo la kisasa anasema tayari upo mpango wa kuanzisha njia za safari kutoka stendi ya mabasi Kibaha kwenda Bagamoyo na Kibaha kwenda Kisarawe.
 
 Afisa huyo anaeleza fursa nyingine katika Manispaa hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli ya nyota tano katika eneo la karibu na stendi ya mailimoja ambapo anawaalika wawekezaji kujitokeza kufanya uwekezaji.


 Akizungumzia kuhusiana na uwekezaji wa viwanda ambao umefikia 368 anasema ongezeko hilo la viwanda linaendana sambamba na watu ambao wanahitaji kupata nyumba za kunga na kwamba tayari wametenga eneo kwa ajili ya uwekezaji wa nyumba za makazi.


 Fursa nyingine aliyoitaja ni ua ujenzi wa vyuo vya ufundi ambapo amewaita wawekezaji kufika katika manispaa hiyo kwani tayari eneo la ujenzi limetengwa katika kata ya Pangani na kwamba vyuo hivyo vitakuwa kimbilio kwa vijana wengi ambao wanahitaji kufanya kazi kwenviwanda vilivyopo ndani na nje ya Manispaa hiyo.


 “Taasisis zinazojenga ofisi na wawekezaji tunawaalika kufika kununua na kutumia tofali zetu ambazo ni imara na zitawafaa katika ujenzi wenu, wafanyabiashara pia tunawaalika kuchangamkia fursa kwenye fremu zilizojengwa katika kata ya Picha ya Ndege, Mkuza na Kongowe hizi ni sehemu salama kwa biashara zenu,” anasema.
 
 Anawasisitiza wakazi wa Manispaa ya Kibaha na maeneo ya jirani kuchangamkia uwekezaji kwenye maeneo yaliyoainishwa sambamba na kufungua biashara kwenye fremu zilizojengwa ili kujikwamua na umasikini , kuinuka kiuchumi na kukuza pato la familia na taifa kwa ujumla.