Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani ni kati ya taasisi zilizopo mkoa wa Pwani ambazo zimekuwa na mafanikio katika kutimiza majukumu yake ya kukusanya mapato ya serikali.
TRA Mkoa wa Pwani inajivunia kukua kwa mapato ya serikali kutokana na usimamizi madhubuti wa sheria za kodi, huduma bora, ubunifu na uwazi katika utoaji wa huduma pamoja na urahisishaji wa mifumo ya ukusanyaji kodi. Pia tunajivunia uimarishwaji wa dhana ya ushirikishwaji wa walipakodi na elimu ya kodi ambayo inatolewa kwa mlipakodi ili aone umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati kwa maendeleo ya Taifa.
Uongozi wa TRA Mkoa wa Pwani umeelezea kuwa taasisi hiyo imekasimia jukumu la kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya serikali. Jukumu hili muhimu la kusimamia kwa uadilifu kodi mbalimbali za serikali kuu, huwezesha serikali kupata fedha za kuhudumia jamii na kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa.
Uongozi huo pia umesema ili TRA iweze kukusanya mapato hayo ya serikali zipo sheria mbalimbali ambazo wanazisimamia. Pamoja na jukumu hilo kubwa la kukadiria na kukusanya mapato ya serikali pia wana jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kwani wanaamini mwananchi aliyeelimika atajua manufaa ya kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati.
"TRA kama taasisi tumekuwa tukiwekeza nguvu kubwa kwenye kutoa elimu kwa wananchi na katika kufanikisha hili taasisi yetu ina idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano," ulisema uongozi huo.
TRA Pwani, imesema mwananchi aliyeelimika na akajua manufaa ya kulipa kodi na akajua kwanini analipa kodi ni rahisi kulipa kodi kwa hiyari bila kutumia nguvu jambo ambalo taasisi hiyo imekua ikiwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu na ushirikishwaji wa mlipakodi.
Anasema kwamba Taasisi hiyo pia wana jukumu la kuwezesha biashara, ambapo kwa idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa kuna kitengo maalum cha kuwezesha biashara; kazi yake ikiwa ni kuwafanya wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa urahisi na kuhakikisha biashara zinaimarika.
"Tunaamini kwamba kwa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara itawezesha biashara hizo kukua na kuimarika na hivyo kuongeza mchango wao kwa Taifa.
Kwa upande wa idara ya Kodi za Ndani kuna kitengo kinaitwa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara (Trade facilitation Unit – TFU) dawati hili lina jukumu la kushirikiana na wafanya biashara kutatua changamoto zao kwa ufanisi, kuwezesha urasimishaji wa biashara na kuwaunganisha wafanyabiashara na wadau muhimu wa biashara. "unaeleza uongozi huo.
Na ili kuhakikisha lengo hilo linatimia kila mlipa kodi anapoleta barua ya kufunga biashara wanafanya juhudi za kumtafuta ili kujua ni kwa nini anafunga biashara na ikibainika changamoto ni ya kikodi wanatafuta namna ya haraka kuitatua.
Pia uongozi huo umesema kama mfanyabiashara anataka kufunga biashara na changamoto inahusishwa na taasisi nyingine wanatafuta namna ya kukutana na taasisi hiyo kujadiliana na kumaliza tatizo na kumuwezesha mfanyabiashara huyo kuendelea na biashara yake.
"Kupitia dawati hilo pia tunalo jukumu la kuifikia sekta isiyo rasmi, kwa sababu kuna watu ambao wanahitaji kuwezeshwa mitaji kwa kuchukua mikopo na unakuta mtu huyo hayupo kwenye sekta rasmi, tunachofanya tunamuwezesha kwa kumpa Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (Tax Identification Number- TIN) na Cheti cha Umahili wa Kodi (Tax Clearance Certificate) ili kumsaidia kwenda kwenye taasisi za kifedha kupata mikopo na akishaanza kufanya biashara na kukua anaanza kulipa kodi," uongozi huo lifafanua.
Uongozi huo ulienda mbali zaidi na kusema kuwa "Unakuta mwingine pia sio kwamba anataka kukopa, mfano kama sasa hivi kuna vikundi vinapewa tenda za serikali kwa kwa mujibu wa sheria kila taasisi inatakiwa kutenga asilimia 30% ya fedha yake ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalumu na ile fedha wanatakiwa watumie vikundi vya vijana, wanawake, wenye ulemavu na wazee kufanya yale majukumu, kwa hiyo wakati mwingine unakuta hawajasajiliwa tunawawezesha".
Mamlaka hiyo imekuwa ikikutana na vikundi ambavyo vimesajiliwa kwenye Halmashauri na kuwapatia elimu na wakati mwingine wanavikusanya na kutafuta mtaalamu wa mambo ya masoko na benki na wanapewa elimu ya kuangalia fursa zilizopo ili waweze kukua.
Kuhusu uanzishwaji wa dawati la uwezeshaji biashara, TRA Pwani imeanzisha Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara ambalo ni maelekezo ya serikali yakiwa na lengo la kuwezesha wafanyabiashara na biashara kukua zaidi kwa kutatua changamoto mbalimbali za kikodi na zisizo za kikodi, ili kusaidia ukuaji wa biashara kwa kuwa daraja kati ya serikali na wadau mbalimbali kwenye biashara na kuboresha utii wa taratibu kwa kurahisisha huduma zetu pamoja na kutoa elimu ya biashara na kodi"
Hata hivyo uongozi huo ulimshukuru Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndugu Yusuph Juma Mwenda kwa usimamizi makini na hasa kusimamia kwa dhati dhana ya uwezeshaji biashara, ushirikishaji walipakodi kwenye masuala mbalimbali ya kikodi na utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi ili kusaidia kuongeza uwajibikaji na uwazi kwenye mifumo ya kikodi.
Kuhusiana na jukumu kubwa linalofanywa na Taasisi hiyo anasema kazi yao ni kuhakikisha kodi sahihi za Serikali zinakusanywa na kazi hiyo inapofanyika kwa usahihi kuna faida kubwa kwa nchi.
Kitendo cha kulipa kodi ni ishara ya uzalendo lakini pia kodi inapolipwa ni sehemu ya kuitegemeza nchi ili iweze kujitegemea .
"Wote ni mashahidi tumemsikia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema kuwa tunahitaji kujitegemea kwa kutumia rasilimali zetu za ndani kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Kila mmoja anahitaji kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Rais kwa kulipa kodi sahihi na kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, kukuza uchumi na kuleta maendeleo," ulisema uongozi huo.
Pia kila mmoja anapotekeleza jukumu lake la kulipa kodi unaifanya nchi isitegemee sana misaada ya nje kwani mingine imekuwa ikija na masharti ambayo wakati mwingine yanatweza hadhi ya nchi.
Uongozi ulisisitiza kuwa kila mmoja akilipa kodi anaisaidia Serikali kupeleka huduma kwa wananchi ikiwemo miundombinu ya elimu kama vile kujenga madarasa, maabara, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu, kwenye afya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali, kununua vifaa tiba na dawa; kadhalika ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na barabara, kulipa mishahara ya watumishi wa umma na kuimarisha ulinzi wa nchi.
Mkoa wa Pwani umekuwa ukikua kwa kasi kutokana na nafasi ya kimkakati ya mkoa ambao ni kitovu cha viwanda.
Kuongezeka kwa uwekezaji ndani ya mkoa wa Pwani kunatokana na kuwa na mazingira mazuri na rafiki yanayowavutia wawekezaji.
Pia kumekuwa na jitihada kubwa zinazofanywa na wadau mbalimbali ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo MKuu wa Mkoa wa Pwani, Ndugu Abubakari Kunenge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila taasisi inaweka mazingira rafiki ili kuvutia uwekezaji ndani ya mkoa wetu.
Moja ya sababu za wawekezaji kuvutiwa na kuja kuwekeza Tanzania ni utulivu wa kisiasa kwenye nchi yetu na ukarimu wa watanzania ambao unawafanya wawekezaji wengi kufikiria kuwekeza hapa Tanzania kwa sababu kuna uhakika wa usalama wa mitaji yao.
Kila taasisi mkoa wa Pwani ina jukumu la kuhakikisha inawawezesha uwekezajii na kwa kufanya hivyo inakuwa mmoja ametimiza jukumu na wajibu wa kuvutia uwekezaji ndani ya mkoa. Vivyo hivyo TRA kama taasisi ndani ya mkoa wa Pwani ina maeneo mbalimbali ya kuvutia uwekezaji ikiwemo kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma bora na kwa wakati ili waweze kuendelea na uwekezaji wao.
Uwekezaji una faida mbalimbali ikiwemo ya wawekezaji wanaozalisha bidhaa na kuziuza nje ya nchi na hivyo kusaidia serikali kupata fedha za kigeni kwa kuuza bidhaa lakini wapo ambao wanazalisha bidhaa ambazo zilipaswa kununuliwa kutoka nje na hiyo pia inasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Wawekezaji hao pia wanapokuja wanasaidia kutengeneza ajira kwa vijana, uwekezaji ndani ya mkoa wa Pwani unasaidia pia kuanzishwa kwa biashara nyingine na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya mkoa .
Aidha uongozi wa TRA Pwani, ulibainisha kuwa mfumo unaotumika kukusanya kodi za Forodha na Ushuru wa Bidhaa TANCIS umeimarishwa sana huku ukiweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na walipakodi.
Pia kuna Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ambao umekamilika kujengwa na kuanza kutumika rasmi tangu mwezi Februari 2026. Mfumo huu utaimarisha usimamizi wa sheria za kodi, ulipaji wa kodi kwa usawa na kupunguza migogoro kati ya walipa kodi na mamlaka.
Mfumo huu pia utaunganishwa na taasisi 300 kwa hiyo ili kuweza kupata taarifa nyingi kutoka kwenye taasisi hizo na hivyo walipakodi kukadiriwa na kulipa kodi ambazo ni sahihi.
Mfumo huu utawawezesha walipakodi na wadau wote kupata huduma za TRA masaa 24 kupitia mfumo huu na hivyo kupunguza kutumia muda wa kuja ofisini kupata huduma na hivyo kuwapa walipakodi muda wa kutosha kufanya biashara zao.
“Swala la watu kulalamika kwamba wakati mwingine wanakadiriwa kodi ambayo sio sahihi litapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kuondoka kabisa kwa sababu kutakuwa na taarifa sahihi," ulifafanua zaidi uongozi huo.
Hata hivyo, uongozi huo ulitoa shukurani za kipekee kwa Serikali kwa kutoa fedha ili kujenga mfumo huo wa kisasa na hivyo TRA itaendelea kutoa kila msaada unaohitajika ili kila mmoja aweze kunufaika na mfumo huu.
Ofisi ya TRA Pwani imejipanga kwenye eneo la kutoa elimu kwa kila Afisa kuhakikisha anatoa elimu kwa kila mlipakodi anayekutana nae maana wanaamini kuwa wanapowekeza kwenye elimu walipakodi wengi wataelimika na hivyo kuwa rahisi kulipa kodi kwa hiari.
Ili kuwafikia wafanyabiashara wadogo TRA imeanzisha utaratibu wa kampeni ya mlango kwa mlango ambapo hufika kwenye kila duka kwa nia ya kuangalia kama mfanyabiashara amesajiliwa na analipa kodi sambamba na kusikiliza changamoto zao kwa ajili ya utatuzi.
TRA Pwani, imetenga kila siku ya Alhamisi kwa ajili ya kuwasikiliza wafanyabiashara na kutatua changamoto zao.
TRA mkoa wa Pwani pia inajivunia ongezeko la mapato katika vipindi tofauti ikiwemo cha 2023/2024 na 2024/2025 ambapo ukuaji wa makusanyo ulifikia Tshs. Bilioni 55.16 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 91.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED