Ni mkoa wa kimkakati unaoongoza katika uwekezaji wa viwanda na ili kuendelea kuwavutia wawekezaji, maboresho katika sekta mbalimbali yanafanyika ikiwemo kwenye miundombinu ya barabara.
Kwenye Barabara mkoa wa Pwani unahudumiwa na taasisi mbili, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na wakala wa Barabara (TANROADS).
TARURA mkoa wa Pwani inasimamia na kuhudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya km.5,188.649 ambazo ni barabara za zinazotumiwa na magari kutoka barabara moja kwenda barabara kuu km 1779.126(34.29), barabara zinazounganisha eneo moja na lingiine mfano kwenye mitaa 2,723.838 (52.49) pamoja na barabara za jamii zenye urefu wa km 685.685(13.22).
Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani Ibrahim Kibassa akizungumza na Nipashe anabainisha kwamba mkoa huo una barabara za lami km 122.41 (asilimia 2.36), changarawe km 871.392 (asilimia 16.79) na barabara za udongo ni km 4179.948 (80.55).
TARURA PWANI NA MAFANIKIO
Meneja Kibassa anaeleza mafanikio wanayojivunia kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami kutoka km 64.144 mwaka 2020 hadi kufikia km 122.41 mwaka 2026.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa barabara za changarawe kutoka km 588.773 mwaka 2020 hadi km 871.392 mwaka 2026, na pia mtandao wa barabara za udongo zimepungua kutoka km 4593.022 kwa mwaka 2020 hadi km 4,179.948 kwa mwaka 2026.
Mhandisi Kibassa anaeleza mafaniko mengine kuwa ni pamoja kuongezeka kwa idadi ya makaravati kutoka 2,294 mwaka 2020 hadi 3590 mwaka 2026,madaraja 13, maboksi kalavati 148 na madrafti 43.
Mfanikio mengine ni kuongezeka kwa mtandao wa barabara kutoka km sifuri kwa mwaka 2020 hadi km 10.55 mwaka 2025 sambamba na kuweka taa za barabarani kutoka sifuri mwaka 2020 hadi taa 1014 mwaka 2026.
Utekelezaji wa bajeti 2024/2025
TARURA mmoa wa Pwani ilitengewa bajeti ya bilioni 28,054,691,827.81.
Mhandisi Kibassa anaainisha shughuli zinazoendelea kufanyika kupitia bajeti hiyo ambazo ni pamoja kujenga barabara za lami km 3.1 barabara za changarawe km 286.62 karavati mistari 130 maboksi kalavati tisa na mifereji 3,245 na kufunga taa za barabarani 111 na kufanya matengenezo ya barabara km 1226.78.
Kadhalika TARURA imepokea bajeti ya miradi kutoka Benki ya Dunia (CERC) yenye thamani ya bilioni 20.4 ambayo inaendelea kutumika kujenga barabara za lami km 6, kujenga boksi karavati 19, karavati 81 na mifereji mita 12,500.
Kazi nyingine zinazofanyika kupitia fedha hizo ni pamoja na kujenga barabara za changarawe km 35 na kuweka taa za barabarani 200.
Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026
Katika mwaka wa fedha 2025/2026 ilipitishwa kiasi cha bilioni 29.4 ambayo inakwenda kujenga barabara za lami km 3.96, barabara za changarawe km 351.82 kujenga karavati mistari 77, maboksi karavati matatu, mifereji mita 38,180 na kufanya matengenezo ya barabara km 966.27.
Utekelezaji wa miradi ya uondoaji wa vikwazo vya barabarani kwa kutumia fedha kutoka Benki ya Dunia.
Katika Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe ipo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ikiwemo ya boksi karavati katika barabara ya Mzenga-Gwata ambao unatekelezwa na kampuni ya Neloyt kwa thamani ya milioni 359.6 ambao umefikia asilimia 10 ya utekelezaji.
Mhandisi Kibassa anasema ujenzi wa boksi karavati katika barabara ya Kisarawe – Kwembe unatekelezwa na kampuni ya Old South kwa gharama ya milioni 314,450 ambao umefikia asilimia 65 ya utekelezaji wake.
Vilevile Meneja anaeleza kwamba upo mradi wa matengenezo ya sehemu korofi katika barabara ya Chole-Kihare ambao unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya Judex kwa mkataba wa kiasi cha milioni 250,990 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 75, kwa thamani ya sh. milioni 338,113,480 na mradi huo umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake.
Kadhalika anaeleza kwamba katika Halmashauri hiyo upo mradi wa ujenzi wa boksi karavati katika barabara ya Kwala- Mperamumbi km 10.82 ambao unatekelezwa ba kampuni ya Yesaca Civil and Building Works kwa thamani ya milioni 414,724,600 na umefikia asilimia 60 ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kibasa katika Wilaya ya Rufiji ipo miradi sita inaendelea ukiwemo wa ujenzi wa boksi karavati katika barabara ya Mohoro-Mtanga ambao unatekelezwa na kampuni ya M/S Jonenac Construction kwa gharama milioni 340,315 na umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake.
Mradi mwingine unaotekelezwa katika wilaya hiyo ni ujenzi wa boksi karavati katika barabara ya Mohoro –Kipoka unaotekelezwa na kampuni M/S Jonenac Construction ambao una thamani ya milioni 778,955 na umefikia asilimia 35.
Upo pia ujenzi wa barabara ya Nyamwage-Mpakani ambao unatekelezwa na kampuni ya M/S Investment kwa thamani ya bilioni 2.4 na hadi sasa umefikia asilimia 25 ya utekelezaji.
Katika Wilaya ya Rufiji pia upo ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira inayojengwa kwa kiwango cha changarawe unatekelezwa na kampuni ya M/S Osaka kwa thamani ya bilion 1.3 na kwasasa umefikia asilimia 2.
Katika utekelezaji wa miradi hiyo ya kuondoa vikwazo barabarani kwenye Wilaya hiyo pia upo mradi wa ukarabati wa barabara wa barabara ya Ikwiriri –Mtanange ambao unatekelezwa na kampuni ya M/S Morcep Investment kwa thamani ya milioni 830,180 na hadi sasa umefikia asilimia 52.
Pia ujenzi wa lami na mifereji katika mji wa Ikwiriri unaendelea ukitekelezwa na M/S Afritrust Group kwa thamani ya bilioni 6.3 na umefikia asilimia 40, huku ujenzi wa lami katika mji wa Utete unaotekelezwa na M/S Fesam Construction kwa thamani ya bilioni 1.3 ambao hadi sasa umefikia asilima 5.
Katika mradi huo unaotekelezwa kupitia fedha za Benki ya Dunia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, ujenzi wa mifereji Kibiti mjini unaendelea ukitekelezwa na kampuni ya Rabco Construction kwa gharama ya bilioni 1.9 na sasa umefikia asilimia 15.
Vilevile katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mradi wa boksi karavati mbili katika barabara ya Mbezi-Shungubweni –Boza (mto Galawani na tuta la Boza ) unatekelezwa na kampuni ya Mponela Construction kwa mkataba wa thamani ya milioni 922.8 umefikia asilimia 20.
Pia ujenzi wa boksi karavati na unyanyuaji wa tuta katika barabara ya Sotele-Nasibugani-Mavunja (bonde la Mavunja) unatekelezwa na kampuni ya Pamvic kwa mkataba wa thamani ya sh. 1,073,375,000 ambao umefikia asilimia 30.
Mbali ya miradi hiyo katika Wilaya ya Mkuranga pia upo ujenzi wa boksi kalavati mbili barabara ya Vikindu –Sangatini utekelezaji unaofanywa na kampuni ya Ubaruku Construction kwa mkataba wenye thamani ya bilioni 1.3 hadi sasa umefikia asilimia 95.
Kwa mujibu wa Meneja Mhandisi Kibassa Wilaya ya Chalinze kuna mradi wa uchukuaji wa hatua za dharura katika barabara ya Vigwaza – Mbuyuni unaotekelezwa na kampuni ya Higo Investment kwa mkataba wenye thamani ya milioni 192.5.
Miradi ya fedha maalum
Meneja Kibassa anaeleza kwamba Serikali kupitia TARURA mkoa wa Pwani iliingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya MAC kwa ujenzi wa daraja la Mohoro katika barabara ya Mohoro- Kipoka Wilaya ya Rufiji kwa gharama ya bilioni 17.8 hadi sasa bilioni 7.4 tayari zimelipwa huku mradi ukiwa umefikia asilimia 54 ya utekelezaji.
Mhandisi Kibassa anaongeza kwamba upo mradi wa barabara ya Utete-Kingupira kwa kiwango cha lami (km 2) pamoja na matengenezo ya sehemu korofi km 30 ambao unaendelea kutekelezwa na mkandarasi RABCO kwa gharama ya bilioni 2.5 na tayari umefikia asilimia 40.
Utekelezaji mradi wa TACTIC
Anaeleza kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 Manispaa ya Kibaha inatekeleza mradi wa TACTIC unaohusisha matengenezo ya barabara ya Tughe-Anglikana (km 1.1) na barabara ya Picha ya Ndege –Lulanzi Hospitali- NDC (KM 3.7) kwa kiwango cha lami.
Kadhalika kupitia mradi huo upo uboreshaji wa bustani ya mapumziko na ujenzi wa soko la mnarani pamoja na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu wa mradi ambao ulianza Novemba 2025 unaotarajiwa kukamilika Feb. 2027.
Mradi huo ambao unafadhiliwa na shirika la Maendeleo la Kimataifa (IDA) la Benki ya dunia kwa gharama ya bilioni 19.8 na unatekelezwa na Mkandarasi Dimetoclasa Real Hope ambaye tayari amelipwa fedha za awali kiasi cha bilioni 2.9 na kwa sasa mradi upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Mpango wa ujenzi wa barabara zinazoelekea kwenye viwanda
Kutokana na mkoa huo kuendelea kuwa kinara katika ujenzi wa viwanda wa bidhaa mbalimbali Tarura imejipanga kuondoa changamoto za barabara kurahisisha usafirishaji kwa kutambua barabara zinazoelekea kwenye viwanda hivyo.
Mhandisi Kibassa anasema tayari wameandaa andiko la mahitaji ya miundombinu ya barabara katika maeneo ya viwandani kutokana na kwamba barabara nyingi za udongo hazihimili usafirishaji wa mizigo mikubwa.
Kwasasa mkoa wa Pwani una km 12.6 ya barabara za lami katika eneo la Zegereni, km 3.3 za lami katika eneo la NDC Kibaha na Km 18.6 za barabara za zege katika eneo la Kwala huku maeneo mengine yakiwasalia kuwa na kiwango cha changarawe na udongo.
Kutokana na hali hiyo TARURA mkoa wa Pwani imeandaa makisio ya ujenzi wa barabara katika maeneo ya viwanda zikipangwa kwa kiwango cha changarawe lengo likiwa ni kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa za viwandani unafanyika kwa ufanisi ambao utagharimu trakribani kiasi cha bilioni 47.5.
Aidha upembuzi yakinifu umeanza kufanywa katika baadhi ya barabara kwa ajili ya uboreshaji kufikia kiwango cha lami na njia hiyo inaelezwa kwamba itahakikisha kila barabara muhimu za viwanda zitatimiza mahitaji ya usafiri wa bidhaa kwa muda mrefu na ubora wa kimataifa.
Tarura imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara ambazo zimeleta manufaa kwa wananchi kurahisisha usafiri na usafirishaji , kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED