BoT yatunza tani 28 za dhahabu kuimarisha uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:24 PM Jul 07 2026
 Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Picha: Mpigapicha Wetu
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68, sawa na shilingi trilioni 9.76, katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, thamani ya shilingi, uthabiti wa sekta ya fedha na ukuaji wa uchumi.

Hayo yamesemwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, wakati akishiriki mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu wa Benki Kuu (Central Bank Gold Operations) katika Mkutano wa African Caucus 2026, unaozihusisha nchi 54 za Afrika na unaofanyika jijini Banjul, Gambia.

Tutuba amesema mpango huo umeiwezesha Tanzania kuongeza akiba ya dhahabu kama mbadala wa kutunza fedha za kigeni, sambamba na kuimarisha urasimishaji wa sekta ya madini na kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu.

Amesema kupitia mpango huo, BoT imewawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kufungua zaidi ya akaunti 4,000 katika taasisi mbalimbali za fedha, hususan benki, hatua inayochochea ushiriki wao katika mfumo rasmi wa kifedha.

Aidha, Gavana huyo amesema bei shindani inayotolewa na BoT imeongeza mwitikio wa wachimbaji na wafanyabiashara kuiuzia benki hiyo dhahabu.

“Tunawalipa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kwa wakati, ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa mauzo, na tunawalipa kwa bei ya soko la dhahabu la London ya siku hiyo. Hii imekuwa kivutio kikubwa kwao kuiuzia dhahabu Benki Kuu,” amesema Tutuba.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, na unawajumuisha Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anayehudumia pia shughuli za kibalozi nchini Gambia, Balozi Selestine Kakele.

Mkutano wa African Caucus 2026 umewakutanisha viongozi wa Afrika, watunga sera, wataalamu wa masuala ya fedha, washirika wa maendeleo na wawakilishi wa taasisi za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kujadili masuala ya maendeleo ya uchumi, usimamizi wa madeni, biashara, ajira, mabadiliko ya tabianchi na mageuzi ya sekta ya fedha barani Afrika.