Mahakama ya Wilaya ya Same leo imewapandisha kizimbani watuhumiwa saba wanaokabiliwa na mashitaka mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya aina ya mirungi, huku mtuhumiwa mmoja akiwekewa amri ya kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi kwa miaka mitatu.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakamani, jumla ya kesi saba zimefunguliwa, kila moja ikimhusu mtuhumiwa mmoja. Washtakiwa wote walisomewa mashitaka yao na wakayakana, ambapo mashauri yao yameahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi ya kwanza, Goodlak Bariki Mungulu anashtakiwa kwa kupatikana na mirungi yenye uzito wa kilo 1.8. Shtaka hilo liliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Jackson Matowo, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Christanta Chitanda. Mshtakiwa alikana shtaka hilo na shauri lake limepangwa kutajwa tena Juni 24, 2026. Pamoja na kuwa na haki ya dhamana, ameshindwa kutimiza masharti yaliyowekwa.
Kesi ya pili inamhusu Athuman Tuarira Kivuma, anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha mirungi kilo 27. Naye alikana shtaka hilo, na shauri lake limepangwa kutajwa tena Juni 24, 2026.
Katika kesi ya tatu, Nuru Mbonea Mndeme anashtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 25. Mashitaka yake yalisomwa mbele ya Hakimu Chitanda, naye alikana. Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Februari 24, 2026.
Kesi tatu nyingine zilisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hellen Hozza. Katika mashauri hayo, Youze Eliwaha Kitua anashtakiwa kwa kusafirisha mirungi kilo 34, Ahadi Mbazi Mnjama kilo 26, na Edson Elihazina Kibaja kilo 24. Mashitaka yao yaliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Alex Rusibamayila. Washtakiwa wote walikana tuhuma hizo, na mashauri yao yamepangwa kutajwa tena Machi 2, Machi 4 na Machi 3, 2026 mtawalia.
Katika kesi ya saba, Mganga Wahidi Dorovu alipandishwa mahakamani kwa ajili ya kuwekewa amri ya kuwa chini ya uangalizi wa Polisi kwa kuzingatia tabia njema. Mahakama iliamuru awe chini ya uangalizi wa Polisi Same kwa kipindi cha miaka mitatu, akitakiwa kuripoti kituoni kila mwezi na kutojihusisha na uhalifu wowote, ikiwemo biashara au matumizi ya dawa za kulevya.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED