Watu wanne wamefariki dunia na wengine 14 wakijeruhiwa katika ajli ya barabarani iliyotokea leo Julai 7, 2026 majira ya asubuhi katika Kata ya Chem Chem mkoani Tabora ikuhusisha basi la abiria lenye namba za usajili T384 DGF mali ya kampuni ya Last Bullet lililokuwa likitoka Mkoani Tabora kuelekea Mkoani Geita.
Akizungumza katika eneo ilikotokea ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Twaha Lulengelule, amesema waliofariki ni mtoto wa mwaka mmoja na watu wazima watatu, majeruhi wakiwa 14.
“Taarifa hii ni ya awali, uchunguzi unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo cha ajili, kwasababu dereva wa basi hilo alitoroka baada ya ajali kutokea,” amesema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa gari hilo lilikuwa na mwendo wa kasi hali iliyosababisha dereva kushindwa kulimudu na kupelekea kuangukia mtaroni, huku wakiziomba mamlaka husuka kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoendelea kugharimu maisha ya wananchi.
Majeruhi wa ajali wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED