Wananchi waua majambazi wanne Mbeya

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 06:17 PM Mar 17 2026
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Watu wanne wanaodhaniwa kuwa majambazi wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na wananchi kwa mawe na silaha za jadi katika mtaa wa Sokoni, Kata ya Uyole jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea Machi 15, 2026 majira ya asubuhi, ambapo wananchi waliwazingira watu hao waliokuwa wakijificha ndani ya nyumba moja.

Amesema watu hao wanadaiwa kuwa sehemu ya kundi la wahalifu waliokuwa wakivizia wananchi nyakati za usiku, kuwapiga nondo, kuvunja nyumba na kuiba mali, huku wakijeruhi baadhi ya wakazi.

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa majira ya saa 4:45 asubuhi kuwa kuna watu wanashambuliwa katika eneo la Uyole, na kikosi maalumu cha kuzuia uhalifu kilitumwa haraka kwa ajili ya kuwaokoa.

Hata hivyo, amesema askari walipofika eneo la tukio walikuta wananchi tayari wamewazingira watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia, na juhudi za kuwaokoa zilikwama baada ya wananchi pia kuanza kuwashambulia askari kwa mawe.

Kamanda Kuzaga amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Erick Nasoro (20), Meshaki Joseph (20), Abdalah Goliam maarufu kwa jina la Sakalani (20) na Asajile Isack (25), wote wakazi wa Sokoni Uyole.

Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.