Usafiri, biashara zasuasua Mwanza,polisi yatoa kauli

By Damian Masyenene , Nipashe
Published at 02:12 PM Jul 07 2026
news
Picha Damian Masyenene
Usafiri, biashara zasuasua Mwanza, polisi yatoa kauli

Kutokana na uwepo wa tishio la maandamano leo Julai 7, baadhi ya shughuli za kiuchumi za kila siku zimedorora kutokana na wananchi kuwa na hofu huku wengine wakishindwa kwenda kwenye majukumu yao huku wafanyabiashara na wajasiriamali wakishindwa kufungua maduka.

Katika siku zingine za kawaida mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza, imekuwa ikifurika watu wakiwemo wajasiriamali wadogo pamoja na maduka yakifunguliwa na usafiri wa umma ukifanya kazi kama kawaida, lakini hali imekuwa tofauti.

Nipashe Digital imeshuhudia baadhi ya mitaa ikiwa tupu, maduka mengi yakiwa yamefungwa, huku machinga na mama lishe wakiwa hawajaingia kazini, wakati huo vituo vya daladala vikiwa na magari machache kuliko ilivyozoeleka.

Hata hivyo, jeshi la polisi limeimarisha doria mitaani likiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa ambaye ametembelea baadhi ya vituo vya bodaboda na kuzungumza nao.

Polisi wakiimarisha doria Mwanza
Akitoa taarifa yake, Mutafungwa amesema jeshi hilo limeimarisha hali ya usalama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za maendeleo.

​Mutafungwa amesema wameimarisha hali ya usalama kwa kuwapanga askari katika maeneo muhimu, lengo kubwa likiwa ni kulinda watu na mali zao.

​Hata hivyo, amewataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote, kwani ni wajibu wa jeshi la polisi kulinda usalama wao.

"Wananchi wasiogope kuona ongezeko la askari mitaani, bali wafurahi kwa sababu uwepo wao ndiyo unaohakikisha usalama wa maisha na mali zao," amesema Mutafungwa.

Polisi wakiimarisha doria Mwanza
​Aidha, Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa watu wenye nia ya kusababisha uvunjifu wa amani kuacha mara moja, kwani Jeshi la Polisi limejipanga imara na yeyote atakayejaribu atadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.

​"Kwa kweli hatutaruhusu mtu yeyote afanye vitendo vya uvunjifu wa amani; atadhibitiwa kisheria na kwa nguvu kubwa," amesema Kamanda Mutafungwa.

​Pia, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha usalama na kufuatilia kwa karibu taarifa za wahalifu zinazotolewa na wananchi wema.

Polisi wakiimarisha doria Mwanza