Simanzi imetanda miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Moshi kufuatia kifo cha mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa kampuni inayojishughulisha na masuala ya ujenzi Bosco Chuwa, aliyefariki dunia Julai 5, 2026 baada ya kuugua ghafla.
Mwenyekiti wa Kambaita katika Kata ya Soweto, Agnes Lyimo, amesema alimfahamu Chuwa tangu mwaka 2002 na kwamba alikuwa jirani yake na mmoja wa watu waliokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii.
Alisema alimfahamu Bosco Chuwa tangu mwaka 2002 kama jirani yake, na kwamba alikuwa mtu muhimu sana katika mtaa wao.
“Tulifanya naye kazi kipindi cha ulinzi shirikishi ambapo alikuwa mdau mkubwa. Pia alikuwa mwanachama na mdau muhimu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Soweto," amesema Lyimo.
Amesema Chuwa alikuwa mstari wa mbele kusaidia jamii, hasa pale wananchi walipokabiliwa na changamoto za kiuchumi.
“Alikuwa akitubeba sana wakati wa changamoto mbalimbali za kiuchumi. Kifo chake kimetushtua na kutuumiza sana. Tulipopata taarifa hizo jana tulienda nyumbani kwake na familia ikathibitisha kuwa ni kweli. Ilikuwa ni wakati mgumu kwetu, lakini tukajipa moyo kwa kuwa hiyo ni safari ya kila mmoja,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya familia nyumbani kwa marehemu eneo la Soweto, Manispaa ya Moshi Julai 6, msemaji wa familia, Allan Mtowe, amesema Chuwa alifariki Julai 5 baada ya kuugua ghafla akiwa barabara.
"Aliamka akiwa na afya njema, ila baadaye mchana alijisikia vibaya alipokuwa njiani kuelekea mjini. Alisimamisha gari pembeni na kuwasha taa za tahadhari.
“Watu waliokuwa karibu waliona amekaa kwa muda mrefu ndani ya gari, ndipo wakawasiliana na mmoja wa watoto wake, Junia Bosco, ambaye alifika eneo hilo," amesema Mtowe.
Amesema mtoto huyo alimkuta baba yake akiwa katika hali mbaya na akaanza jitihada za kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu.
"Madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake, lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia. Familia ilikutana Julai 5 na imekutana tena leo Julai 6 kuendelea na maandalizi, huku ikitarajia kutoa taarifa Julai 7 kuhusu tarehe na mahali atakapozikwa," amesema.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni yake, Wenzesilaus Urio, amesema kuwa Chuwa alikuwa mwajiri aliyependa kazi yenye ubora na aliyewapa nafasi vijana.
"Mzee alikuwa mbunifu, alipenda vijana wafanye kazi na alikuwa na msimamo. Hakupenda uzembe na alithamini utu wa watu aliokuwa akifanya nao kazi," amesema Urio.
Baadhi ya mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Moshi akiwemo, Babu Frank amesema Chuwa alikuwa mtu mwenye ukarimu wa kipekee.
Amesema walifurahia kupewa kazi katika maeneo ya Chuwa kutokana na namna alivyowajali na kuzungumza nae
"Ukija kazini ukaambiwa unaenda kufanya kazi maeneo ya Bosco, ulikuwa na uhakika wa kula, kunywa na hata kurudi nyumbani ukiwa umepewa mkate. Alikuwa mtu mwema sana na alitujali," amesema
Naye, Jackson Herman amesema Chuwa alikuwa na moyo wa kusaidia mafundi hata alipokutana nao njiani.
"Hata akikukuta njiani na akajua wewe ni fundi, alikuwa anakupa chakula na ushauri. Kwetu sisi hiki ni pigo kubwa sana," amesema
Chuwa alikuwa mmiliki wa Builders and Lime Works Construction Company Ltd, kampuni inayojihusisha na uzalishaji wa chokaa pamoja na ujenzi wa barabara kwa kutumia mitambo yake katika maeneo mbalimbali nchini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED