Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni Dar es Salaam, kimewakusanya wasichana na wanawake walea pweke (anaolea watoto pekee yao) na kuwapa elimu kuhusu msaada wa kisheria na elimu ya afya ya uzazi.
Wasichana na wanawake hao pia wamepata msaada wa kisaikolojia na elimu ya fedha ili wanapopata mitaji waweze kuitumia vizuri katika biashara na kupata faida ya kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Seleman Bishagazi amesema wamekusanya kundi hilo ili kuadhimisho nalo Siku ya Wanawake Duniani ambayo waliifanya jana na kualika wasichana na wanawake 46.
"Hili ni kundi linalopitia madhila na mikasa mbalimbali linapotafuta huduma muhimu za watoto wao. Ni kundi lililotengwa na jamii. Ni kundi linalolaumiwa na waliotakiwa kulitia moyo," amesema Bishagzi.
Amefafanua kuwa wasichana hao na wanawake wanaolea watoto pakee bila wazazi wa kiume, ni kundi lisilofikiwa na fursa, lakini pia linazidi kuongezeka kwa kasi, linalea watoto wenye hasira kwa baba zao.
"Kundi hili linazidi kuongezeka kila uchao. Sisi tulialika walea pweke 46, lakini wamekuja 120, lakini pia tunajiuliza hawa watu tukiwatenga watapata msaada wapi? Kumbuka kwamba linalea watoto ambao ni viongozi wa baadaye, hivyo ni muhimu kulisaidiam," amesema.
Bishagazi amesema hakuna binti aliyekuwa na ndoto ya kuzaa akiwa na umri mdogo au kuzaa na kutelekezwa na mzazi mwenzake au familia,na kwamba wenye madhila kama hayo wanatakiwa kutiwa moyo.
Katika maadhimisho hayo, Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Kipunguni, Tumaini Urio amesema ni muhimu msichana au mwanamke kujua mbinu mbalimbali zitakazomsaidia kufanya maamuzi sahihi.
"Kwa elimu walioipata hapa, ninaamini itawasaidia katika mambo mengi yakiwamo ya kutambua ni wakati gani wazae au watu wa kuzaa nao ili kuepuka mazingira ya kulea watoto pekee yao," amesema Tumaini.
Mmoja wa wanawake wanaolea watoto pekee yao, Debora Simon, kutoka Msongola, amesema alishakumbana na vikwazo vya kutopata msaada kutoka kwa familia ya mzazi mwenzake wakati mtoto anaumwa.
"Niliambulia matusi kutoka kwa shangazi zake mtoto wangu, hadi leo nikimwambia aende akawasalimie hataki, anasema hawezi kwenda kwa watu walionitukana," amesema Rose.
Amesema wanawake wanaolea watoto pekee yao wananyanyasika na kwamba mafunzo aliyopqta kutoka Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni yamempa ari mpya ya kujiamini.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED