Samia: Kodi zisipendelee wala kukandamiza watu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:51 PM Mar 18 2026
Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesema mapendekezo ya Tume aliyoiunda ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi, yanashauri kuwepo kwa utulivu katika ulipaji wa kodi wafanyabiashara.

Mkuu huyo wa nchi, amefafanua kuwa Tume hiyo inapendekeza sera za ulipaji wa kodi ziwe zimetulia na zinazotekelezeka, sambamba na kuwa na tafsiri moja ya kisheria inayoeleweka.

“Sio sheria ambazo mfanyabiashara akisoma kifungu hicho hicho anauelewa tofauti na mkusanyaji wa mapato akisoma kifungu hicho hicho anauelewa tofauti. Tuwe na sheria ambayo kifungu kinachosema kisimame hivyo hivyo kwa mfanyabiashara na mkusanyaji wa kodi,” ameeleza Dk Samia.

Rais Dk Samia ameeleza hayo leo Jumatano Machi 18,2026 wakati   akipokea ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Lakini kwa upande mwingine kodi zetu ziwe ‘neutral’ hazikandamizi watu wala kupendelea watu. Ziwe neutral mfanyabiashara afanye shughuli zake, alipe kodi na Serikali ikusanye mapato,” amesema nakuongeza kuwa:

“Pia zisiumize wale ambao wale ambao… lakini ziwe kodi zinazokuza biashara na mapato nchini. Lakini jingine kodi zitutoshe na kuendelea kuongeza wigo wa ukusanyaji,” ameeleza Dk Samia.