Nguzo zege kuimarisha huduma umeme

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:25 PM Mar 12 2026
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgallu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha nguzo za zege kinachomilikiwa na kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kilichopo mkoani Tabora.

Kamati hiyo imetembelea kiwanda hicho Machi 12, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya nishati inayotekelezwa na shirika hilo.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgallu, amesema kamati imeridhika na hatua ya kukamilika kwa kiwanda hicho ambacho tayari kimeanza uzalishaji.

Ametoa rai kwa Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO kuhakikisha wanasimamia kiwanda hicho ili kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi na kuzalisha faida.

“Kwa niaba ya Kamati tumeridhika na kazi kubwa iliyofanyika katika kiwanda hiki ambacho kimekamilika na uzalishaji umeanza. Tunatoa rai kwa Wizara na TANESCO kuendelea kukisimamia ili kifanye kazi kwa ufanisi zaidi,” amesema Mgallu.

Ameongeza kuwa kwa sasa uelekeo ni kusambaza nguzo za zege badala ya nguzo za miti, hasa katika maeneo yenye unyevu mwingi, maeneo yaliyo karibu na misitu pamoja na mikondo ya mito, ambapo nguzo za miti huathiriwa kwa kiasi kikubwa hususan wakati wa msimu wa mvua.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa kiwanda hicho ulikamilika mwaka huu na uzalishaji rasmi ulianza Februari 2026.

Amesema kwa sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha kati ya nguzo 80 hadi 120 kwa siku. Hadi kufikia hatua ya uzalishaji, jumla ya shilingi bilioni 6.4 zimetumika katika ujenzi wa kiwanda hicho, huku takribani shilingi bilioni 1.4 zikiwa bado hazijalipwa kwa mkandarasi ambaye yupo katika kipindi cha uangalizi wa mradi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutaleta mageuzi makubwa katika upatikanaji wa nguzo za umeme nchini.

Amebainisha kuwa matumizi ya nguzo za zege ni teknolojia inayokua kwa kasi, hivyo shirika hilo linaendelea kuimarisha sekta hiyo ili kuhakikisha kunakuwa na utoshelevu wa nguzo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

“Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda na kuanza uzalishaji, TANESCO itaendelea kusimamia sekta hii ili kuwapatia wateja huduma ya umeme wa uhakika,” amesema Twange.