Mtoto anajisiwa na kuuawa, mwili watelekezwa jirani na kwao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:50 PM Mar 09 2026
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Allan Bukumbi.

Hali ya taharuki imetanda miongoni mwa wakazi wa eneo la Isakalilo katika Manispaa ya Iringa baada ya watu wasiojulikana kumnajisi mpaka kumuua mtoto mmoja aitwaye, Naomi Kivamba (13) kisha kuutelekeza mwili wake jirani na nyumbani kwao.

Mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Zizi la Ng’ombe iliyopo katika kata ya Isakalilo Manispaa ya Iringa.

Baba mdogo wa mtoto huyo, Benjamin Kikula amesema marehemu aliondoka nyumbani siku ya Jumamosi majira ya saa 9:00 alasiri baada ya kutumwa dukani na kaka yake kwenda kununua kiberiti na kwamba tangu muda huo hakurudi tena nyumbani.

Ameeleza kuwa familia ilitoa taarifa kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Njia Panda  kuhusu kupotea kwa mtoto huyo na juhudi za kumtafuta zilianza kufanyika kwa kushirikiana na wananchi wengine wa mtaa huo.

“Tulipigiwa simu na jirani yetu ajulikanaye kwa jina la Kalinga mida ya sa tatu asubuhi siku iliyofuata akituambia kuwa mwili wa mtoto umeonekana   jirani na  nyumba yao,”  amesema Kikula.

Amesema walipofika eneo hilo walimkuta mtoto akiwa tayari amefariki dunia huku mwili ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye paja na shingo ikiwa imevunjwa.

Mwenyekiti wa mtaa wa Njiapanda, Maisha  Modestus amesema tukio hilo limewashitua  na tayari taarifa zimetolewa kwa vyombo vya Dola ili uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa

Aidha Modestus   ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda watoto wao na kuepuka kuwaacha wazurure ovyo akisisitiza kuwa watoto hawapaswi kuonekana nje ya nyumba zaidi ya saa 12 jioni bila sababu maalum.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Allan Bukumbi amesema  Machi 8, mwaka huu  walipokea taarifa za mauaji  ya mtoto huyo na wanaendelea na upelelez wa tukio hilo ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua.

Bukumbi amesema mwili wa mtoto huyo ulipatikana  ukiwa umepigwa na kitu chenye  ncha Kali hali ambayo ndiyo iliyosababisha kifo chake..

Mazishi yamtoto huyo yanatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Mawambala wilayani Kilolo.